Taarifa kuhusu habari ya mgonjwa wa Ebola kutoka Tanzania

Nimelazimika kuandika taarifa hiii baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa ndugu yangu kupitia WhatsApp akinitaka kusoma habari iliyomtia hofu baada ya kuisoma kwenye blogu moja inayomilikiwa na Mtanzania.
Nami nimeisoma mistari michache na kutafuta chanzo chake ambacho kinaonesha habari yenyewe iliandikwa mwezi uliopita, haipo kwenye vyombo vikubwa vya habari (yaani vyombo rasmi vilivyosajiliwa na vinavyoaminiwa kwa habari zake - registered and authentic) lakini tayari leo blogu kadhaa zinazomilikiwa na Watanzania zimeanza kuisambaza kama ilivyo.

Habari hiyo iliyochapishwa na tovuti moja inadai kuwa yupo mgonjwa nchini
 Marekani katika jimbo la Georgia mwenye asili ya Tanzania ambaye amegundulika kuwa mgonjwa wa pili kuugua ugonjwa unaosababishwa na virusi hatari wa Ebola.
Habari hiyo ambayo inasema mgonjwa huyo aligundulika kuugua Ebola baada ya kurudi kutoka nchi yake ya asili, Tanzania, na kupelekwa katikahotpiali ya Grady Memorial, ni ya mzaha na haipaswi kuchukuliwa kwa makini kwani mwishoni kabisa kwa tovuti hiyo pameandikwa, “NewsBuzzDaily.com is a combination of real shocking news and satire news. Please note that articles written on this site are for entertainment and satirical purposes only.”

Maneno hayo yanajieleza wazi na kumfahamisha yeyote anayesoma habari za tovuti hiyo kuwa taarifa zake ni za mzaha na burudani .

Mara kwa mara tunaendelea kukumbushwa kuwa makini kwa kuchunguza habari, taarifa na maandiko ili kupembua ukweli dhidi ya uongo na kuacha kusambaza habari ambazo zinaweza kusababisha mtafaruku katika jamii usio na sababu hata kidogo.

Tafadhali ukikutana na habari hiyo, ipuuze.

Post a Comment

Previous Post Next Post