Al-Shabaab yawateka wakaazi, yawakata kichwa wanawake 2 huko Kudha
Na Fuad Ahmed, Mogadishu
Al-Shabaab waliwakata vichwa wanawake wawili na kuwateka zaidi ya raia
20 iliowatuhumu kwa kufanya ujasusi na kupinga mitazamo yao baada ya
kukimata kwa muda kisiwa cha Kudha tarehe 8 Novemba.
Wanamgambo wa al-Shabaab walifanya msako
nyumba hadi nyumba kisiwani Kudha, wakawakusanya wasichana na wavulana
iliowatuhumu kuifanyia ujasusi Serikali ya Mpito ya Jubbaland. Pichani
juu, wakaazi waliokimbia majumba yao Bulomarer wanaweza kurudi tarehe 31
Agosti baada ya wanajeshi wa Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia
kuukomboa mji huo kutoka kwa al-Shabaab. [Picha ya AMISOM / Tobin Jones]
"Ninaweza kuhakikisha kwamba wanawake hao wawili waliokatwa vichwa na
al-Shabaab na zaidi ya raia 20 waliowateka hawakuhusika hata kidogo na
tuhuma walizowatwisha za kuifanyia ujasusi Serikali ya Mpito ya Jubba
(IJA)," alisema Kanali Urdan Kilas Gurase wa vikosi vya usalama vya IJA.
"Wanawake hao walikuwa na umri wa chini ya miaka 20 na kile kinachofanywa na hawa jamaa ni ushenzi," aliiambia Sabahi.
Al-Shabaab iliikimbia Kudha siku ya Jumatatu (tarehe 10 Novemba), siku
tatu baada ya kukishambulia kisiwa hicho na kuwauwa kiasi cha wanajeshi
15 wa IJA.
Vikosi vya IJA sasa vimerudi kuchukua udhibiti wa kisiwa hicho, alisema Gurase.
Wanamgambo wa al-Shabaab walikuwa wamefanya msako wa nyumba kwa nyumba
kwenye kisiwa hicho na kuwasafirisha raia iliowateka hadi kwenye maeneo
yasiyojuilikana, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Somalia.
Wakaazi wengi wa Kudha waliyakimbia maeneo ya mbali wakihofia ukatili wa al-Shabaab, alisema Gurase.
"[Wanamgambo hao] wanawadhuru wananchi kwa sababu wamekasirishwa na
namna raia walivyofurahia hasara yao. Kile raia hawa wanachokitaka ni
kuwa huru dhidi ya magaidi ya al-Shabaab," alisema.
Akizungumza kutoka Kismayu, kiongozi wa wazee wa Kudha, Omer Jeylani
mwenye umri wa miaka 50 aliiambia Sabahi kwamba watu wanahofia hali
zinazowakabili marafiki na familia zao walioko nyumbani.
"Kitu kinachotuhofisha sana ni pale tuliposikia wanawake wawili wasio
hatia wamekatwa vichwa katikati ya Kudha na taarifa za zaidi ya watu 20
hazifahamiki baada ya al-Shabaab kuwachukua," alisema Jeylani.
"Tunadhani nao pia wamewachinja."
Imekuwa ni shida kuwasiliana na watu wa Kudha kwani al-Shabaab imekata mitandao ya mawasiliano, alisema Jeylani.
"Ni vigumu kwetu kuwasiliana na jamaa zetu huko, na watu hawatwambia
mengi tunapowapata (kwa simu)," alisema. "Wanahofia kwa sababu
al-Shabaab wameingia kwa nguvu kwenye nyumba nyingi na kuwachukuwa watu
ambao taarifa zao bado hazijuilikani."
Mkaazi wa Kismayu, Maryam Mumin, mwenye umri wa miaka 61, alisema binti
yake na watoto sita wa binti huyo bado wako Kudha na kwamba anahofia ni
vipi wataweza kuvuuka.
"Tunaishi kwenye siku za giza la kutokujua kama wazazi juu ya waliokwama
kisiwani Kudha kwa sababu al-Shabaab wanalipiza kisasi kwa yeyote
aliyevipokea vikosi vya serikali ya Jubba wakati wao (al-Shabaab)
walipofukuzwa kutoka kisiwa hicho," aliiambia Sabahi.
"Mungu atulinde na al-Shabaab. Ni watu waovu," alisema.
Mumin alivitolea wito vikosi vya Umoja wa Afrika na IJA kuhakikisha
kundi hilo "haliwezi tena kuyakamata maeneo waliyoyachukuwa kutoka kwa
magaidi hao."
Wakati vikosi vya Somalia vikichukuwa udhibiti wa ngome za zamani za
al-Shabaab, serikali ya shirikisho inawahimiza wananchi kuripoti
shughuli zozote zinazotilika mashaka na wapiganaji wa al-Shabaab
waliosalia kujisalimisha wenyewe na kutumia fursa ya programu ya msamaha
iliyoongezwa muda hadi mwishoni mwa mwaka huu.
"Kuna njia ambazo kila mwanamme, mwanamke na mtoto anaweza kupambana na
magaidi hawa pia; na hakuna hata moja kati ya njia hizo inayojumuisha
kukamata bunduki," alisema Rais Hassan Sheikh Mohamud mwezi uliopita.
"Badala yake, tunaweza kushika simu na kuripoti vitendo vya kutilika
mashaka na vya kihalifu serikalini," alisema. "Hilo linaweza kumaanisha
kuwa tunamripoti jirani au binami yetu, kaka au dada yetu, hata mtoto
wetu wa kiume au wa kike - lakini tutakuwa tunawaokoa, na pia kuokoa
maisha ya Wasomali wasio hatia."
Chanzo: sabahionline.com
Post a Comment