BARAZA
la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), limesema kuwa halitaacha kuwaeleza
wananchi mapungufu yaliyopo kwenye Katiba Pendekezwa kwani Rais JakayaKikwete ndiye aliyeanza kampeni kabla ya wakati ya kuhamasisha wananchi kuipigia kura ya ndiyo.
Aidha, limesema likimaliza ziara hiyo ya kanda ya Ziwa Magharibi,
watarudi bungeni kuihoji serikali sh bilioni 2.5 zinazotarajiwa kutumiwa
na Ikulu kwenye vyombo vya habari kushawishi kura ya ndiyo zinatoka
kwenye fungu gani na zilipitishwa na bunge lipi.
Hayo yalisemwa juzi na Mbunge wa Viti Maalum, Suzani Lyimo, wakati
akiwahutubia wananchi wa Tarime kwenye uwanja wa Serengeti akiwa
ameambatana na Makamu wa BAWACHA Taifa, Hawa Mwaifunga, Katibu Grace
Tendega, Naibu Katibu Kunti Yusuph, wabunge wa viti maalum Ester Matiko,
Grace Kiwelu na Chiku Abwao.
Alisema kuwa, Rais Kikwete ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuanza kampeni
ya kuipigia chapuo katiba pendekezwa, kwani hata wakati akipokea mwenge
wa Uhuru aliwasisitiza wananchi kuipigia kura ya ndiyo kwa madai kuwa
ni nzuri.
“Labda wachukue sindano na uzi watushone midomo yetu vinginevyo
tutaendelea kuwaeleza wananchi ubovu wa Katiba pendekezwa…Rais Kikwete
akipokea Mwenge wa Uhuru tulimsikia akifanya kampeni waziwazi,
akiwaambia wananchi kuwa katiba pendekezwa ni nzuri na ikifika wakati wa
kuipigia kura wasiache kuipa kura zote za ndiyo,” alisema Lyimo.
Alisema kuwa, inashangaza kuona wakati Rais akidai kuwa muda wa
kampeni kwa ajili ya katiba bado, lakini viongozi wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), wameweka hadharani nyaraka zikionyesha kuwa Ikulu
wanatenga sh bilioni 2.5 kwa ajili ya kuendesha kampeni ya kura za ndiyo
kupitia vyombo vya habari.
“Tukirudi bungeni tutaenda kuhoji hizi sh bilioni 2.5 zinatoka kwenye
fungu gani na zinatolewa kwa utaratibu upi, wakati kwenye bajeti
tuliyopitisha ya mwaka 2014/2015 wa fedha suala hili halikuwepo,”
alisema Lyimo huku akishangiliwa na wananchi.
Tendega aendelea kulia michango ya maabara
Katibu wa BAWACHA, Grace Tendega, alisema kuwa wataendelea kupinga
wafanyakazi wa umma kukatwa mishahara yao bila kuridhia kwa ajili ya
kuchangia ujenzi wa maabara mpaka serikali itakapofuata sheria.
Alisema kuwa, hawapingani na ujenzi wa maabara lakini wanachokataa ni
utaratibu unaotumika kukusanya fedha za ujenzi huo ambao umegeuka kero
kwa watumishi wa umma na wananchi maskini wa vijijini, ambao wengine
huwalazimu kukimbia makazi yao kujificha kutokana na hali ngumu ya
uchumi inayowakabili.
“Narudia tena kusema kama kweli Rais Kikwete ana nia ya dhati na
mpango huu wa ujenzi wa maabara kwenye shule za kata, basi apunguze
bajeti yake ya sh bilioni 50 aliyotengewa kwa safari za nje ya nchi,
aipeleke ikatekeleze ujenzi huo,” alisema Tendega.
Kunti ataka Polisi wanaoua wananchi Tarime wachukuliwe hatua
Naibu Katibu wa BAWACHA Taifa, Kunti, alisema kuwa inasikitisha kusikia kuna wananchi wanaouawa na polisi huko Nyamongo maeneo ya kuzunguka mgodi wa dhahabu wa North Mara, lakini hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa dhidi yao.
Naibu Katibu wa BAWACHA Taifa, Kunti, alisema kuwa inasikitisha kusikia kuna wananchi wanaouawa na polisi huko Nyamongo maeneo ya kuzunguka mgodi wa dhahabu wa North Mara, lakini hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa dhidi yao.
Alisema kuwa kazi ya polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao,
hivyo inapotokea polisi wanaua raia ni lazima wachukuliwe hatua za
kisheria, kwani hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kutoa uhai wa
Mtanzania na kikanyamaziwa, kwani nchi inaendeshwa kwa utawala wa
sheria.
“Tunataka wale wanaoua vijana wetu kule Nyamongo, wachukuliwe hatua
za sheria wafikishwe mahakamani kwa makosa ya mauaji, hatukubaliani na
mauaji ya aina hii kwenye Taifa huru na tunawaahidi wana Tarime tuko
tayari kuungana na nyie kuandamana mpaka mgodini kupinga mauaji haya
wakati wowote mkituhitaji,” alisema Kunti.
CHADEMA wampiga marufuku Makonda kukanyaga Mara
Katibu wa CHADEMA mkoani Mara, Chacha Heche, amemtaka Kiongozi wa
Chipukizi wa UVCCM, Paul Makonda, kuwaomba radhi Watanzania kwa vitendo
vya utovu wa nidhamu alivyomfanyia Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph
Warioba, vinginevyo asikanyage mkoa huo.
Alisema kuwa haiwezekani vijana wa Tanzania kunyamazia vurugu
alizofanyiwa kiongozi huyo Mstaafu aliyelitumikia Taifa kwa uadilifu
kutokana na misimamo yake ya kutetea maslahi ya umma kwenye rasimu ya
katiba, hivyo akasisitiza kuwa kama Makonda hataomba msamaha basi aishie
eneo la Rubana mpakani mwa mikoa ya Mwanza na Mara.
Matiko ahoji uprofesa wa JK aliopewa China
Mwenyekiti wa BAWACHA mkoani Mara, Ester Matiko, alisema kuwa
uprofesa aliopewa Rais Kikwete nchini China, unaibua maswali mengi hasa
ukizingatia tuhuma nzito zilizoibuliwa hivi karibuni na vyombo vya
habari vya kimataifa vya BBC kuwa msafara wa rais wa China, Xi Jinping
uliokuja nchini mwaka jana uliondoka na pembe za ndovu.
Matiko ambaye pia ni mbunge wa viti maalum, alisema kuwa utata wa
uprofesa huo unazidi kuibua maswali hasa ikizingatiwa kuwa wakati Rais
huyo wa China alipofika hapa nchini alisaini mikataba 28 ya gesi na
mafuta ambayo mpaka sasa ni siri, hata wao kama wawakilishi wa wananchi
hawaijui.
Ziara ya BAWACHA kanda ya Ziwa Magharibi mpaka sasa imetumia siku 21,
ambako wamefanya mikutano kwenye mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu
na Mara.
Post a Comment