Katuni
Taarifa kwamba serikali imeamua kuunda timu hiyo zilitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mjini Dodoma katika ibada ya kumweka wakfu Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika ya Kanisa Anglikana, zinaonyesha kwamba sasa inaamka kutambua kwamba kuna shida.
Kulingana na kauli ya Waziri Mkuu, timu hiyo itakuwa ni mchanganyiko wa watu kutoka kada mbalimbli, miongoni mwao ni viongozi wa dini. Moja ya majukumu ya timu hiyo ni kupata usuluhishi na maridhiano katika maeneo ambayo kumekuwa na mapigano.
Waziri Mkuu alisema serikali inataka kutumia Kiteto kama mfano (pilot project) kwa nia ya kujenga amani, maridhiano ili mafanikio yake yatekelezwe pia maeneo mengine ya nchi ambako kumekuwa na matatizo yanayofanana na hayo.
Ni dhahiri kwamba Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyojaliwa ardhi kubwa yenye rutuba. Ukubwa wa Tanzania ni km za mraba 945,087. Ukubwa huu ni sawa na kuziunganisha kwa pamoja Kenya yenye ukubwa wa km za mraba 580,000, Uganda km za mraba 241,038, Burundi yenye km za mraba 27,834 na Rwanda yenye ukubwa wa km za mraba 26,338 na kubakia km za mraba 69,877karibu sawa na ukubwa wa Georgia yenye ukubwa wa km za mraba 69,700.
Pamoja na ukubwa wa Tanzania hadi sasa ina jumla ya watu milioni 45 tu. Kwa ukubwa Tanzania ni ya 31 duniani na kwa idadi ya watu ni ya 28 duniani.
Ukitafakari ukubwa wa nchi na idadi ya watu unaweza kushangaa kuona kwamba mataifa mengi yaliyopiga hatua za maendeleo kama vile Japan pamoja na kuwa na eneo dogo la km za mraba 377,915 ina watu 127,080,000 ikishikilia nafasi ya 10 kwa idadi ya wingi wa watu; Ujerumani ambayo ilitutawala kabla ya kufurushwa na wakoloni wenzake kutokana na vita kuu ya kwanza ya dunia, ina watu 80,767,000 huku ikiwa na ukubwa wa km za mraba 357,022.
Ndivyo ilivyo kwa Uingereza yenye ukubwa wa km za mraba 242,900 ikiwa na watu 64,105,654 na Ufaransa yenye ukubwa wa km za mraba 551,500 na idadi ya watu 66,050,000.
Mataifa yote tuliyoorodhesha hapo juu yamepiga hatua kubwa sana za maendeleo, ni miongoni mwa yale tuliyoyabatiza jina la nchi wahisani au wafadhili. Yaani zina nguvu kubwa za kiuchumi na zina ziada ya kutoa misaada kwetu kwa miaka yote 53 ya uhuru wetu.
Kimsingi huwezi kusikia mapigano juu ya ardhi kwenye hayo mataifa tuliyotaja kuwa ni wahisani. Huwezi kusikia kwa sababu moja kubwa, kwanza wamekwisha kuvuka hatua ya uchumi tegemezi kama wa kwetu; lakini la umuhimu wa kipekee sana ardhi kwao ni rasilimali muhimu, imepangwa na kuwekewa utaratibu wa kisheria, kanuni na mipangilio ambayo hairuhusu vurugu na fujo.
Ni dhahiri kama Tanzania ni kubwa zaidi ya Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Georgia kwa pamoja, kusikia eti kuna watu wanapigana kwa sababu ya ardhi, kitu pekee kinachoweza kuelezwa kuwa chanzo cha hali hiyo ni mipango mibovu juu ya matumizi ya ardhi.
Haiwezekani eti wakulima na wafugaji wapigane mwaka mzima, katika mabonde ya Kilosa, Kiteto, Handeni, Kilindi na kwingineko kama kweli taifa hili lipo makini kwamba ardhi ni rasilimali na ni lazima ipangwe na isimamiwe vizuri katika matumizi yake.
Ingawa serikali inataka ionekane kuwa inafanya jambo la maana sasa juu ya mapigano ya wakulima na wafugaji, kimsingi viongozi wenye dhamana katika maeneo ya usimamizi wa ardhi, ulinzi na usalama walipaswa wawe wamekwisha kujiuzulu.
Chimbuko la mapigano ya wakulima na wafugaji siyo kitu kingine chochote isipokuwa ni sera mbovu na sheria mbaya za kusimamia matumizi bora na endelevu ya ardhi.
Pamoja na timu ya watu 10 ambayo serikali imeahidi kuwa inaunda kusaka mwafaka wa mauaji na madhila yote ya Kiteto, inapaswa kujielekeza kwenye swali gumu kama sheria za ardhi za nchi hii ni bora kiasi gani.
Kwa hali hiyo itajua kuwa zinataka kufanyiwa kazi ili zijibu changamoto za sasa na zijazo. Hakuna manufaa yoyote yatakayopatikana kama sheria za sasa za ardhi hazitaguswa.
Haiwezekani kwamba kwa ukubwa wa Tanzania na uchache wa watu wake, eti ardhi iliyoko haitoshelezi mahitaji ya watu wake kwa sasa. Ni lazima serikali itambue kwamba ardhi ndiyo msingi wa haki zote za maendeleo. Kwa hali hiyo, ni lazima ijifunze kwingineko duniani ambako wamefanikiwa. Kuendelea kupiga domo tu na kuunda timu kwa kuwa kuna shida Kiteto leo, ijue kwamba haitatatua tatizo hili.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment