
Juma Kaseja
Hata hivyo, Kaseja amedumu mwaka mmoja tu Yanga na kitendo cha kukaa benchi kimemfanya ashindwe kuitwa kwenye timu ya Taifa (Taifa Stars).
Akizungumza na NIPASHE jana, Meneja wa Kaseja, Abdulfatah Saleh, alisema wameamua kuvunja rasmi mkataba na Yanga kwa sababu Kaseja hakuwa na raha katika kipindi chote alichokuwa akiitumikia timu hiyo ya Mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam.
Abdulfatah alisema leo anatarajia kukutana na viongozi wawili wa Yanga, Seif Ahmed 'Magari' na Isaac Chanji ili kujadili mkataba wa Kaseja lakini ameweka wazi kuwa hatakubali kuzungumzia kumaliza tofauti zao.
Meneja huyo alisema hata kama Yanga itakuwa tayari kumlipa Kaseja kiasi cha fedha kilichoandikwa kwenye mkataba au zaidi, mazingira ya klabu hiyo hayajamfurahisha kipa huyo ambaye alikuwa chaguo la kwanza Simba na Taifa Stars kwa kipindi kirefu.
Alisema mara kadhaa Kaseja alidaiwa kuihujumu Yanga jambo ambalo lilikuwa linamnyima raha na kuona kuwa usajili wake kwenye timu hiyo umemuondolea furaha ya maisha yake ndani na nje ya soka.
"Mazungumzo ya awali na Simba yamefanyika, sasa tunatarajia kukutana na Seif na Chanji ili tumalizane rasmi kisheria, ila tunaenda kwenye kikao hicho kesho (leo) huku msimamo wetu ukiwa kuachana na Yanga, hata wakisema wako tayari kumalizana kwa kumlipa Juma (Kaseja) kiasi walichotaka kumpa au mara mbili yake, kwa hilo hatuko tayari," alisema meneja huyo.
Alieleza kuwa yeye pia alikuwa anakerwa kuhusishwa na madai ya kuihujumu Yanga kwa kuwa karibu na wachezaji wa timu hiyo akiwamo kiungo wao kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima.
"Kuna makundi na hawapendani Yanga, nimeshangaa kiongozi mmoja ambaye alikuwa na timu Bukoba (jina tunalo) aliposema mimi ninawahujumu na niliwakatia tiketi za ndege Juma na Niyonzima, wakati tiketi hizo zimekatwa na klabu kutokana na wachezaji hao kila mmoja kuwa na dharura ya kifamilia," Abdulfatah aliongeza.
Kuhusiana na mazungumzo na Simba meneja huyo alisema yanakwenda vizuri na hana wasiwasi.
Abdulfatah alisema kuwa mkataba wa Kaseja na Yanga ulivunjika rasmi kuanzia Novemba 8, mwaka huu kutokana na uongozi wa klabu hiyo kushindwa kumlipa fedha za usajili kama walivyokubaliana hapo awali.
Uongozi wa Yanga ulikubaliana kumsajili Kaseja kwa dau la Sh. milioni 40, na ilimpa awamu ya kwanza Sh. milioni 20 mwaka jana na kiasi kingine kilichobakia ilipaswa kumalizia tangu Januari mwaka huu lakini hadi jana hakuna kilichotekelezwa.
Licha ya kusajiliwa Yanga, mara nyingi Kaseja akiwa kwenye Uwanja wa Taifa kama timu yake haichezi, hukaa upande wa Simba (eneo la VIP B) akiwa sambamba na meneja wake, wachezaji wa Simba ambao hawachezi au marafiki zake.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment