Ninazilinganisha kauli hizi na zile za mzazi
asiyewajibika, ambaye badala ya kutafuta suluhu kwa matatizo au majibu
sahihi ya maswali machache au mengi anayoulizwa na wanae, huishia
kuwapiga makofi, kuwatisha kwa lengo la kuwanyamazisha.
Hakuna shaka, huu ni uwajibikaji wenye kasoro,
ambao kwa kiasi kikubwa unanichochea nifungue midomo yangu na
kuzizungumzia kasoro hizo kwa uchungu.
Nimekuwa nikifuatilia kwa mfano baadhi ya kauli tata ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi wetu, zinanichosha.
Ziara za Katibu mkuu wa chama tawala (CCM), Kanali
Abdulrahman Kinana zimekuwa zikiendelea katika maeneo mengi ya nchi
yetu zikiacha nyuma mifano hai inayochekesha.
Ninamheshimu Kinana, akiwa mtendaji mkuu wa CCM,
ni mtu makini ambaye nimeambiwa na watu walio karibu na ofisi yake kuwa
anajitolea zaidi, kwamba anaishi bila kutegemea chama chake kwa
mshahara, ninampongeza kwa dhati!
Ninaamini, huo ni uzalendo halisi, tena wa kipekee
kwa mtu au kiongozi kuishi bila kujichotea fedha kutoka kwenye ruzuku
ya chama chake ambayo hata kama ni mamilioni kwa mwezi, lakini chama
hiki kinao viongozi wengi ,mtandao mkubwa ulioenea kote nchini, wenye
kutaka fedha nyingi ili kuishi.
Hata hivyo, katika ziara hizo ambazo Kanali Kinana
amekuwa akifuatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye,
nimeshangazwa wakati mwingine na baadhi ya kauli zenye malalamiko,
ambazo hazina majibu.
Nitazungumzia chache, hasa zile ambazo zinahusu
utendaji duni wa Serikali, ile ile ya chama tawala, CCM ambayo imekuwa
ikikumbushwa wajibu wake na wanaofanya hivyo ni Kinana na Nape wakiwa
kwenye ziara hizo, ninawashangaa.
Najiuliza, kwa mfano wanapoitaka ichukue hatua ili
kumaliza matatizo kama ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji kule
Kiteto, mkoani Manyara au kwingineko nchini, wamejiuliza hiyo ni
serikali ya chama gani?
Nilidhani, badala ya kutoa maelekezo katika ziara
zile kwa Serikali, Kinana na Nape wangeitisha mikutano ya viongozi wa
Serikali kwa ruhusa ya mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete waelezane wapi
wamekosea, nini kifanyike ili kumaliza matatizo kama ya Kiteto.
Si mara ya kwanza kuzungumzia utendaji duni wa
Serikali, kwani kauli ya mawaziri mizigo ilianzia kwenye ziara zao,
lakini hakuna hatua thabiti zilizochukuliwa ili kuhakikisha mizigo hiyo
inatoswa baharini, kama ni safari ya meli au jahazi ili kunusuru chombo
katika hatari ya kuzama.
- Soma Zaidi Mwananchi
- Soma Zaidi Mwananchi
Post a Comment