
Maoni ya Katuni
Jitihada za kupambana na biashara hiyo zimekuwa mara nyingi zikigonga mwamba kutokana na sababu mbalimbali. Mojawapo ni kwa waliokamatwa na madawa husika kutopelekwa mahakamani, wakati mwingine upelelezi kuchukua muda mrefu sana, na cha ajabu wakati mwingine vielelezo navyo hupotea kitatanishi.
Katika hatua mbalimbali, serikali imekuwa mstari wa mbele kusimamia utekelezaji wa kudhibiti biashara hiyo ambayo kwa kiwango kikubwa ilikuwa ikifanyikia kupitia viwanja vya ndege nchini, bandari zetu, mipakani na hata wakati mwingine kupitia maiti zilizosafirishwa kuja nchini.
Baadhi ya madawa ya kulevya yaliingizwa nchini kwa ajili ya soko la ndani wakati mengine yalipitia tu yakisafirishwa kwenda nchi mbalimbali duniani, na kwa bahati mbaya sana, wengi wa waliokamatwa nayo ni Watanzania wazawa.
Wiki hii, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akiwa Bungeni amesema serikali inavijua 'vijiwe' vyote vya wauza madawa ya kulevya 'unga' vilivyopo katika mikoa mbalimbali nchini.
Hiyo ni hatua inayotia moyo, ila swali ni je, baada ya kuvijua, hatua zipi zimechukuliwa kuvisambaratisha? Kimsingi, serikali ilitakiwa kuchukua hatua mara moja dhidi ya wamiliki wa 'vijiwe' hivyo ili kudhoofisha mizizi na mtandao wa biashara hiyo unaoendelea kujiimarisha kila siku.
Tunaamini zipo mamlaka maalumu zinazohusika na mapambano hayo ingawa pia zinakwazika kutokana na ugumu unaojitokeza hasa wakati wa kuchunguza kiini na vyanzo vyake.
Waziri Lukuvi aliwaeleza waandishi wa habari Dodoma kuwa serikali inafanya uchunguzi ili kubaini endapo Watanzania waliokamatwa na dawa za kulevya nchini China kama ni Watanzania kwa kuzaliwa au ni watu waliotumia tu pasi za kusafiria za Tanzania.
Lukuvi alikiri uwapo wa Watanzania zaidi ya 80 ambao wamekamatwa nje ya nchi kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya na kufafanua kuwa kati yao, Watanzania 19 walikamatwa nchini China kwa kosa hilo ingawa bado zinafanyika jitihada za kuwatambua kama ni Watanzania au wametumia tu pasi za kitanzania.
Aidha, kati ya Watanzania 80 waliokamatwa nje ya nchi kati ya Januari hadi Desemba 2013, Watanzania 29 walikamatwa nchini Hong Kong, 27 Brazil, watano Kenya na 19 nchini China. Lukuvi akasema baadhi ya Watanzania hao, tayari wamehukumiwa vifungo wakati wengine bado wanasubuiri hukumu.
Maeneo muhimu ambayo ni vituo maarufu vya biashara hiyo ya dawa za kulevya yanayojumuisha mikoa na wilaya nyingi nchini, yalitajwa na Lukuvi na akafafanua kuwa vijiwe vingine vinapatikana kando kando ya barabara kuu zinazounganisha mikoa na vituo vya mabasi na magari makubwa ya mizigo.
Tunaamini kuwa dhamira ya serikali ya kuepukana na aibu hii ya biashara haramu ni ya dhati, hivyo kinachotakiwa ni kila mmoja wetu awajibike kwa kutoa ushirikiano katika mapambano hayo ili hatimaye kulipunguza kama siyo kulitokomeza kabisa nchini.
Serikali ihamasishe wananchi wote kushiriki kikamilifu katika janga hili, majeshi ya ulinzi na usalama yaingilie kati kama ilivyo katika ulinzi shirikishi wa polisi. Ingekuwa ni faraja kubwa endapo wananchi watakaotoa taarifa za wapi na nani wanaofanya biashara hiyo watapewa motisha kuongeza kasi ya kudhibiti janga hilo.
Tunashawishika kwamba hatua za dhati zikichukuliwa dhidi ya biashara ya dawa za kulevya katika vijiwe vyote vilivyotajwa, hatimaye aibu hii ya kuonekana kama Tanzania ni dampo la dawa za kulevya itatoweka. Hili ni janga la kitaifa ambalo ni lazima liwekewe mkakati kulitokomeza hasa ikizingatiwa kuwa kundi linaloathirika zaidi ni vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa letu.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment