Matukio ya hatari yaliyowakumba viongozi wastaafu

Tukio la kufanyiwa vurugu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba hivi karibuni limeshtua makundi mengi ya Watanzania.
Vurugu hizo ambazo mpaka sasa vyombo vya dola vimeshindwa kuweka bayana wahusika wake, zilitokea mwanzoni mwa Novemba katika mdahalo wa kujadili Katiba iliyopendekezwa uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Blue Pearl iliyopo Ubungo mkoani Dar es Salaam.
Vyombo vya habari viliripoti kuwa vurugu hizo zilidumu kwa muda wa zaidi ya dakika 40 na zilitokea baada ya Jaji Warioba aliyewahi pia kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya awamu ya pili, kukemea matumizi ya jina la Mwalimu Nyerere kuhalalisha Katiba inayopendekezwa.
Bado hakuna taarifa rasmi kutoka vyombo vya usalama kuhusu nani hasa aliratibu vurugu hizo, licha ya kuwapo kwa hisia za kuhusika kwa kiongozi wa chama kimoja cha siasa.
Ni kwa hoja hii ya nafasi ya uwaziri mkuu kama mojawapo ya nafasi nyeti katika uongozi wa dola, wananchi wengi wamejitokeza wakipaza sauti zao wakilaani tukio hilo, pia kuhoji usalama wa viongozi wastaafu.
Siyo tukio la kwanza
Hofu ya wananchi wengi kuhusu kadhia hii ya Jaji Warioba kama mmoja wa viongozi mwenye heshima ya kipekee nchini, imekuja ikizingatiwa kuwa kumekuwapo na matukio kadhaa hatari kuhusu usalama kwa viongozi wakubwa nchini.
Mwaka 1972, Tanzania ilishuhudia tukio la kwanza la kushambuliwa kwa kiongozi wa juu serikalini. Huyu alikuwa Rais wa iliyokuwa Serikali ya kwanza ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume aliyeshambuliwa kwa risasi na kusababisha kifo chake katika makao makuu ya Chama cha Mapinduzi, Kisiwandui Unguja.
Rais Karume aliuawa ikiwa ni miaka chini ya 10 tangu aongoze mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa kisultani mwaka 1964. Aliiongoza Zanzibar na kuipa mafanikio ya kiuchumi na kijamii kabla ya shambulio hilo ambalo chanzo chake kiliibua hisia nyingi.
Tukio jingine katika kumbukumbu ni la mwaka 2005 linalomhusu Rais Jakaya Kikwete, kipindi hicho akiwa mgombea wa urais kupitia CCM.
Akiwa katika moja ya mikutano yake jijini Mwanza, alivamiwa na mwananchi jukwaani. Picha za vyombo vya habari vilionyesha mtu huyo alikwenda jukwaani na kumvuta Rais Kikwete kabla ya wasaidizi wake kumtoa msobemsobe eneo hilo.
Baadaye Machi 10 mwaka 2009, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alipigwa kibao na kijana aliyejulikana kwa jina la Ibrahim Said katika hafla ya Baraza la Maulidi iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam

Post a Comment

Previous Post Next Post