
WATU wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti mkoani
hapa, likiwemo tukio la mwanaume mmoja kucharangwa mapanga kwa madai ya
kukutwa akifanya mapenzi na mke wa mtu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Augustine Ollomi, tukio
hilo lilitokea Novemba 3 mwaka huu, Kijiji cha Mnyambe Wilaya ya Newala
mkoani Mtwara, ambako Ali Marunda (34), mkazi wa kijiji hicho aliuawa
kwa kukatwa panga kichwani na begani na Christopher Mtemela (60).
Kamanda Ollomi, alisema kuwa chanzo cha mauaji hayo ni marehemu
kufumaniwa akifanya mapenzi na mke wa mtuhumiwa, ndipo alipoanza
kumshambulia kwa mapanga na kusababisha kifo chake.
Aliongeza kuwa, baada ya mtuhumiwa kufanya mauaji hayo alichukua mwili wa marehemu na kuutupa barabarani.
Mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Katika tukio jingine, Fatuma Abdallah (30), alipoteza maisha baada ya
kukatwa mapanga sehemu mbalimbili za mwili wake na mumewe, Abdallah
Kantunda.
Kamanda Ollomi, alisema tukio hilo lilitokea Novemba 2 mwaka huu
katika Kitongoji cha Rizika, Kijiji cha Kilombelo, Kata ya Mahurunga,
Tarafa ya Kitaya Wilaya ya Mtwara.
Alisema kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alimvizia mkewe alipokuwa
akitokea kisimani kuchota maji na wenzake kisha kumjeruhi kwa kumkata
na panga sehemu za kichwani, shingoni, mikononi na mdomoni, majeraha
yaliyosababisha kifo chake.
Kamanda, alisema mtuhumiwa bado hajakamatwa na juhudi za kumsaka
zinaendelea, kwani baada ya mauaji hayo mtuhumiwa alitoweka na
kukimbilia kusikojulikana.
Post a Comment