Mjadala IPTL wateka kila kona ya nchi

Geita. Maeneo ya migahawa, baa na vijiwe vya kuuza kahawa, katika mji wa Geita vilifurika watu na baadhi ya shughuli zikiwamo za kuchomelea vyuma na vibanda kusimama baada ya wananchi kufurika kwenye runinga kufuatilia mjadala juu ya kashfa ya IPTL uliokuwa ukiendelea bungeni mjini Dodoma.

Maeneo hayo yalianza kufurika saa 10:36 jioni baada tu ya huduma ya umeme uliokuwa umekatika tangu saa 11:05 alfajiri kurejea.

Tangu Jumatano iliyopita huduma ya umeme mjini Geita imekuwa ya kusuasua baada ya kuwa unakatika alfajiri na kurejea jioni hasa muda wa saa 10:30.

Kitendo hicho kimekuwa kikitafsiriwa na baadhi ya wananchi kuwa ni hujuma inayofanywa na Shirika la Umeme Tanesco ili wananchi wasipate fursa ya kujua kinachoendelea bungeni kuhusu mjadala wa IPTL kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow.

Bunge lilianza kujadili kashifa ya IPTL baada ya ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kuwasilishwa na mwenyekiti wake, Zitto Kabwe kwa kupokezana na makamu Mwenyekiti, Deo Filikunjombe na ikitaka baadhi ya viongozi kuwajibishwa akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Wananchi wa mji wa Geita walionekana kuvutiwa na mjadala huo na maeneo hayo yakitawaliwa na ukimya wa hali juu baada ya kila mmoja kukaa kimya kusikiliza mijadala iliyokuwa ikitolewa na wabunge mjini Dodoma.

Mkazi wa Mtaa wa Nyantorotoro, Peter Kombani A, alisema alilazimika kutembea umbali wa kilomita 2, hadi mjini Geita kushuhudia mjadala huo kutokana na eneo anakoishi kutokuwa na huduma ya umeme.

Severine Malugu alisema sakata hilo ni fundisho kwa Watanzania kubadilika na kuchagua viongozi wenye kutetea masilahi ya Taifa na siyo kujali masilahi yao binafsi.

Alisema kiasi cha fedha zilizochotwa zingetosha kujenga maabara nchi nzima, lakini badala yake wananchi wanachangishwa kuhusu ujenzi huo.

‘’Sisi Watanzania njaa zinatusumbua sana lakini bila njaa tungechukua maamuzi magumu ya kuiwajibisha Serikali na viongozi wake. Hili ni fundisho kubwa kwa wananchi wenye ushabiki wa kisiasa wanaotetea viongozi kwa masilahi ya vyama ndiyo tunashuhudia matatizo kama haya,’’ alisema Malugu.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post