Dar es Salaam. Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM),
Nimrod Mkono ambaye hivi karibuni alinusurika kifo akidaiwa kulishwa
sumu akiwa London, Uingereza amesimulia jinsi tukio hilo lilivyomkuta.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkono
alisema endapo uchunguzi wa suala hilo utakamilika na kuthibitisha
kwamba alilishwa sumu, atapambana na wahusika kwa kuwa wamehatarisha
maisha yake.
Mkono ambaye pia ni wakili maarufu nchini, alitoa
kauli hizo jijini hapa jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari kuelezea mwenendo wa afya yake.
Alidai kwamba, lengo la kumlisha sumu ni kuharibu figo zake ndani ya saa 72 wakati alipokuwa katika ziara ya nchini humo.
“Niko vizuri na afya njema… kama kuna mtu anawinda
jimbo langu mwambieni ameshindwa na wananchi wangu nawaeleza kuwa niko
salama wasiwe na hofu. Ninataka kujua nani kanilisha sumu na kwa nini?”
alisema Mkono.
Akisimulia tukio hilo alisema, Novemba 11 akiwa
miongoni mwa wajumbe 11 wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala,
walisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Uingereza akiwa salama salimini.
Aliwataja baadhi ya wabunge walioambatana nao kuwa
ni William Ngeleja (Mwenyekiti wa kamati hiyo), Mbunge wa Temeke, Abbas
Mtemvu, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Utawala Bora), George Mkuchika.
“Tukiwa uwanja wa ndege nilipokea ujumbe mfupi wa
maandishi (hakutaka kuuweka wazi kwa sababu upelelezi haujakamilika),
ukinitahadharisha kuwa makini, ujumbe ule ulinishtua kwa kweli.”
“Niliwaonyesha wenzangu niliokuwa nao na pale
tulikunywa chai kabla ya kuondoka na tulipofika kule mimi nilikaa hoteli
yangu na wenzangu wakakaa ya kwao,” alisema.
Huku akisimama na kunyoosha mikono kuonyesha yuko
vizuri, Mkono alisema siku iliyofuata ratiba iliwataka kuhudhuria Bunge
la Uingereza.
“Niliamka na kwenda Ubalozi wetu na kwa kuwa
tulitakiwa kufika bungeni saa 5.00 asubuhi, niliwahi na wenzangu na
walipokuja tuliungana… tulipokuwa ndani katika Bunge la Uingereza,
ghafla nilianza kujisikia vibaya hali iliyonisababisha nipoteze fahamu
kwa saa sita. “Lakini kabla ya kupoteza fahamu niliwaeleza wanipeleke
nyumbani (Tanzania), wenzangu wanasema nilikuwa napiga kelele,
nirudisheni hawa wanataka kuniua,” alisema Mkono kwa sauti ya chini na
kuongeza:
“Hapa nasimuliwa sasa kuwa walinipeleka
hospitalini na waliponifikisha madaktari wa pale waliamua kuwasiliana
kwanza na Daktari wangu, (Lusangulila Kapitain) ili kujua kama wakati
natoka Tanzania nilikuwa na tatizo.”
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment