Na Bosire Boniface, Garissa
Uvamizi wa hivi karibuni wa misikiti minne uliofanywa na vikosi vya
usalama vya Kenya mjini Mombasa ikituhumiwa kuwa na uhusiano na
al-Shabaab umeibua mchanganyiko wa majibu za umma juu ya kama operesheni
hizo ni mkakati madhubuti wa kupambana na itikadi kali na vurugu.
Maafisa wa polisi wa Kenya wakilinda nje
ya msikiti Swafaa katika wilaya ya Kisauni ya Mombasa kufuatia uvamizi
wa msikiti huo tarehe 19 Novemba, 2014. [PICHA YA AFP / STRINGER]
Siku ya Jumatano (tarehe 19 Novemba), polisi walivamia misikiti ya
Swafaa na Minaa, na kuwatia mbaroni watu 10 na kukamata maguruneti,
risasi na mabomu ya petroli.
Siku mbili kabla, polisi walifanya uvamizi wa asubuhi mapema katika
Masjid Shuhada (uliokuwa ukiitwa Masjid Musa) na Masjid Mujahideen
(uliokuwa ukiitwa Masjid Sakina), wakaua mtu mmoja aliyekuwa akichomea
maguruneti na kuwatia mbaroni zaidi ya watu 250.
Pia walikamata silaha - mabomu sita, bastola kadhaa, risasi, baruti,
mapanga na visu - rekodi za kusikiliza na video juu ya mauaji ya
mwanazuoni mwenye siasa kali Aboud Rogo Mohammed, beji za polisi wa
Kenya, na bendera nyeusi inayohusishwa na al-Shabaab, alisema kamanda wa
Polisi wa Kaunti ya Mombasa Robert Kitur.
Afisa polisi wa Kenya akiteremsha bendera
inayohusishwa na magaidi wa Kiislamu baada ya uvamizi wa misikiti miwili
mjini Mombasa tarehe 17 Novemba. [PICHA YA AFP / STR]
"Operesheni sawia ya usalama ilidumu muda wa saa sita," alisema Kitur
kuhusu uvamizi wa Jumatatu. "Ilikusudiwa kuepusha vitendo vya vurugu
ambavyo vilikuwa vimepangwa kutoka misikiti hiyo miwili na mengine."
Polisi ilikuwa na intelijensia imara kuwa misikiti iliyovamiwa ilitumika
kama maghala ya silaha na kama vituo vya mafunzo kwa shughuli za siasa
kali na vurugu, alisema.
"Operesheni ilikuwa imepangwa kwa mikakati ya hali ya juu kwa karibu
wiki moja ili kuhakikisha kwamba itawanasa wahalifu tuliokuwa tunawataka
zaidi na kuzuia majeruhi kutoka pande zote mbili," aliiambia Sabahi.
Uchunguzi unaendelea
Polisi bado wanachunguza wafungwa na watatolewa wale ambao hawana hatia,
Kitur alisema, akiongeza kuwa watu angalau 40 watafikishwa mahakamani
hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na 24 waliokamatwa katika Masjid
Mujahideen na 16 walikamatwa katika Masjid Shuhada.
Ili kutetea operesheni hiyo, alisema kwamba wahalifu watasakwa popote pale watakapojificha.
"Kujificha katika maeneo matakatifu ni mbinu zinazotumiwa na wahalifu
kuficha shughuli zao na kuanzisha migogoro kutoka kwa waumini dhidi ya
polisi wakati wanapojaribu kuwatoa nje wahalifu," alisema. "Lakini sisi
hatutaruhusu hilo na tutawafuata wahalifu popote."
Polisi pia wanachunguza nia na utambulisho wa kundi la vijana wenye
silaha ambao walifanya ghasia siku ya Jumatatu usiku, na kuua watu wanne
na kujeruhi wengine nane katika kitongoji cha Kisauni.
"Bado hatujui kama tukio hili linahusiana na kukamatwa kwa watu katika
misikiti," alisema Kitur. "Waathirika waliochomwa visu ni Waislamu vile
vile Wakristo na sisi bado tunafanya uchunguzi."
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alisema kuwa watu 110
walikamatwa wakati wa operesheni ya usalama ya Jumatano usiku katika
misikiti Swafaa na Minaa, 36 wameshtakiwa mahakamani.
Aidha, ni mtu mmoja tu aliyekamatwa ndani ya msikiti, alisema.
"Wale waliokuwemo ndani ya misikiti waliparamia kuta na kukimbia wakati
walipopata fununu ya vikosi vya usalama vinakaribia," Marwa aliiambia
Sabahi. "Lakini tumeweza kukamata mabomu ya petroli, maguruneti na
bendera nyeusi inayohusishwa na al-Shabaab."
Mtuhumiwa aliyekamatwa ndani ya msikiti Minaa alishtakiwa katika
Mahakama ya Sheria ya Shanzu akiwa anamiliki panga kwa nia ya kutenda
kosa na alipelekwa rumande chini ya ulinzi na dhamana ya shilingi
300,000 (dola 3,330), Marwa alisema.
Alisema kuwa 33 wengine walishtakiwa kwa uhalifu kuanzia uzururaji na
kukosa vitambulisho, na wote walikuwa huru baada ya kulipa faini za
fedha.
"Mtanzania na Mganda pia walishitakiwa mahakamani kwa kuwemo Kenya
kinyume cha sheria," alisema. "Walitozwa faini ya shilingi 50,000 (dola
555) kila mmoja na watafukuzwa kurejeshwa nchini zao."
Misikiti bado imefungwa
Marwa alisema misikiti minne itabaki imefungwa hadi uchunguzi
utakapokamilika, lakini kwamba vikosi vya usalama vitakuwa katika hali
ya tahadhari kwa uwezekano wa matatizo mjini baada ya sala ya Ijumaa.
"Tupo na tahadhari kwa ukweli kwamba siku ya Ijumaa watu wachache huweza
kuchochea wengine kushambulia maafisa wa usalama wanaolinda misikiti
iliyofungwa," alisema. "Baada ya kusali katika misikiti mengine sala yao
ya Ijumaa, waumini wanashauriwa kutokukaa karibu na misikiti
iliyofungwa kwa sababu hatutavumilia vitendo yoyote vya vurugu."
Msemaji wa polisi wa Kenya Sipora Mboroki alisema polisi mjini Mombasa
wamepewa maelekezo ya kutumia njia zote ziwezekanavyo ili kuhakikisha
amani katika kutakuwa na maandamano ya vurugu baada ya operesheni za
usalama.
"Tumekuwa wapole na kutumia diplomasia wakati tulipotembea katika
operesheni," alisema juu ya uvamizi wa Jumatatu. "Tuliwapa wahalifu njia
rahisi ya kufanya kwa kuacha vurugu zao na kusalimisha silaha
walizokuwa nazo kwetu, lakini wao walikataa masharti yetu. Kwa faida ya
umma mkubwa tulilazimika kuingia ndani."
Mboroki hakutaja idadi ya maafisa wa usalama walioshiriki katika
operesheni, lakini alisema polisi watabaki macho na wataendelea
kufuatilia misikiti. Wakati huo huo, wahalifu lazima wakatishwe tamaa ya
kujificha au kuficha silaha ndani ya misikiti, alisema.
Mboroki aliita operesheni ya Jumatatu kuwa ya mafanikio na kuongeza,
"Wajibu ni juu yetu sasa ili kuhakikisha mafanikio ya kuwashtaki wale
tunaoamini kuwa walihusika katika uhalifu."
Nyumba za Ibada zinastahiki kuheshimiwa
Uvamizi wa misikiti umeibua hisia mchanganyiko kutoka kwa viongozi na wakazi wa eneo hilo.
Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho alisema kuwa anaunga mkono
vikosi vya usalama katika kupambana kwao dhidi ya vitendo vya uhalifu na
ugaidi, ambavyo vinachafua sura na uchumi wa Kenya.
"Wakati majeshi yetu usalama yanapokwenda kusafisha uhalifu nchini
mwetu, pia wanapaswa kuwa na ufahamu wa baadhi ya maeneo kama vile
misikiti," aliiambia Sabahi, akiongeza kwamba vikosi vya usalama na
waumini lazima wayachukulie maeneo ya ibada kwa heshima.
"Kama serikali ingeshauriana na viongozi [wenyeji], pengine tungeweza
kupata njia nzuri ya kupata wahalifu bila ya kulazimika kuharamisha
sehemu za kuabudia," alisema. "Moja ya njia mabazo [tumetumia huko
nyuma] ni kuomba kwa uaminifu sio kuwaruhusu watu kwa kujua kutumia
misikiti kuficha silaha."
"Dini yetu hairuhusu hata [kuleta] silaha msikitini," alisema, akiwaomba raia kushirikiana na serikali kuondoa kabisa uhalifu.
"Natumaini polisi watawahoji kwa kina ambao wamekamatwa kwa sababu
baadhi yao hawana hatia," aliongeza. "Tunaamini kwamba mazungumzo bado
yanaongoza katika [kupambana na] msimamo mkali na serikali inapaswa
kutupatia muda wa kutosha."
Hisia mchanganyiko za umma
Vincent Akama, mwenye umri wa miaka 29, mlinzi binafsi wa usalama huko
Kisauni, alisema uvamizi wa Jumatatu kwenye msikiti ulikuwa "jambo
sahihi kufanyika".
"Ulikuwa ni uamuzi wa kipekee," aliiambia Sabahi. "Unaweza
kushughulikiwa vizuri zaidi, lakini kwa sasa hakika ni uamuzi sahihi kwa
sababu shughuli za msimamo mkali za misikiti miwili zimeandikwa vizuri
na umma unaelewa."
Akama aliwaomba viongozi kufanya uchunguzi wa kina na wale wote
waliokamatwa ili kuhakikisha wasio na hatia wanaachiwa haraka
iwezekanavyo.
"Ninamfahamu jirani yangu Mkristo ambaye alikamatwa wakati wa
operesheni," alisema. "Huuza chai na vitafunwa karibu na msikiti wa
Musa. Kunaweza kuwa na waathirika wengi zaidi kama yeye ambao
wamekamatwa katika tukio hilo."
Athman Hassan Bakari, mwenye umri wa miaka 34, mwendeshaji wa teksi huko
Mombasa, alisema operesheni dhidi ya msikiti imeleta wasiwasi huko
Mombasa.
"Kufunga msikiti haimaanishi kwamba kuna sheria inayowabana raia
watakaoathirika," aliiambia Sabahi, akionyesha wasiwasi kuhusu
uwajibikaji rasmi wa operesheni hiyo.
Lakini Amran Nassir Chiaba, mwenye umri wa miaka 39, mhudumu wa basi
katika kituo cha mabasi cha Kongowea huko Mombasa, alisema uvamizi wa
ghafla wa misikiti unasababisha itikadi kali kumalizika.
"Kitu ambacho serikali ilifanya ni kitu kizuri kukifanya," aliiambia
Sabahi. "Uamuzi wa kuingia msikitini ulipaswa kufanyika mapema kuwaokoa
vijana na Waislamu wengine kupewa hotuba zisizo za Kiislamu."
"Nimehudhuria mahubiri katika misikiti ya Musa na Sakina", alisema.
"Kilichoropokwa kutoka katika mimbari, ni kama imamu alikuwa akitoa wito
wa kutotii sheria za nchi, hakikubaliki."
"Wenye msimamo mkali walikuwa wakipinga serikali kwa muda mrefu na kama
vikosi vya usalama havijafanya chochote kuhusiana na hilo, kungekuwa na
utawala huru," alisema, akiongeza kwamba serikali inapaswa kutafakari
kabla ya kufungua misikiti iliyoifunga.
"Tumekuwa tukikabiliana na vitisho vya ugaidi kwa muda mrefu na lolote linapaswa kufanyika."
Chanzo: sabahionline.com
Post a Comment