SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amepata wakati mgumu wakati wabunge
walipowasilisha hoja kutaka Bunge lijadili suala la haki na maadili ya
Bunge baada ya kuwapo madai kwamba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), imeibiwa ofisini kwa Spika.
Sipika wa Bunge Anne Makinda
Spika Makinda katika jitihada za kuzuia hoja isijadiliwe, alijikuta
aking’aka mara kwa mara hasa baada ya Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa
(CUF), kumtaka aruhusu hoja hiyo kujadiliwa na kwamba, kwenye hizo
nyaraka zinazosambazwa ovyo nje ya Bunge, naye zinamuonyesha ni kati ya
viongozo waliomegewa mabilioni kwenye akaunti ya Escrow.
Hilo lilionekana kumpandisha hasira Spika na kuwaonya watu wanaosambaza
taarifa kwamba naye ni mmoja wa viongozi walimegewa mabilioni ya fedha
kutoka kwenye Akaunti ya Escrow, watakoma.
Spika Makinda ambaye ni mara yake ya kwanza kuongoza Bunge la 16/17
tangu lilipoanza Novemba mwaka huu, kwa mara ya kwanza pia alikutana na
hoja ya kashfa ya kuchota fedha zaidi ya sh bilioni 300 za Akaunti ya
Escrow, zilizohifadhiwa kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na kuibua
mjadala mzito bungeni.
Huku okionyesha dhahiri kuvurugwa na kashfa hiyo, Makinda aliwaambia
wabunge kuwa, watu wanaomchafua kwa kumuingiza kwenye kashfa hiyo,
walete ushahidi vinginevyo watakoma.
Huku wabunge wakiangua kicheko, Spika Makinda alisema anashangazwa na
uvumi huo na kusisitiza ole wao wanaomchafua wakibainika, watakoma.
Makinda alitoa onyo hilo wakati akijibu mwongozo wa Mbunge Mnyaa,
aliyetaka Bunge lijadili hoja ya Mbunge wa kuteuliwa na Rais, James
Mbatia.
Katika hoja yake binafsi, Mbatia alitaka Bunge lijadili suala la haki na
maadili ya Bunge baada ya kuwapo madai kwamba, ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeibiwa ofisini kwa Spika,
imenyofolewa kurasa tatu muhimu na inasambazwa kwa wabunge kama njugu.
Baada ya kutolewa hoja hiyo, iliibuka miongozo mara baada ya kipindi
hicho cha maswali na majibu, ambako Mbunge Mnyaa, aliomba muongozo kwa
kutumia kanuni ya 38(7) kuhusu hoja ya Mbatia, ili ijadiliwe na mjadala
huo ni mpana kwani mmoja wa watuhumiwa wa wizi wa ripoti ya CAG,
amenaswa na Polisi kwa uchunguzi.
“Mheshimiwa Spika, mjadala unahusiana na haki na madaraka ya bunge
kwamba, hivi sasa hali ya Dodoma kwa ujumla wake imechafuka, kuna
nyaraka zinasambazwa, wanatiliwa wabunge nyumbani mwao wanapoishi ambazo
zinawachafua wabunge.
“Mheshimiwa Spika katika kuchafuliwa wameshachafuliwa wengine na hata
hao wa PAC wamechafuliwa na hata wewe umechafuliwa kwamba umechukua dola
milioni moja na inatafutwa ‘document’ kusambazwa ili nawe uchafuliwe,
kwa hiyo naomba hoja ya Mbatia ijadiliwe, japo kwa nusu saa ili wabunge
waweze kulishauri Bunge ili kiti kiweze kuamua.
Akijibu muongozo huo, Makinda alisema; “Tatizo la suala hilo, mnaliweka
wanavyotaka wenyewe na kama nimechukua dola milioni moja, watanionyesha
mfano wake?” mtaonionesha, mtanionesha, mtanionesha in more serious not,
mtanionesha vinginevyo mtakoma…,” na kusababisha wabunge kuibua
vicheko.
Mwingine aliyeomba mwongozo wa Spika alikuwa Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), alisema hoja ya Mbatia kutaka
ijadiliwe bungeni ni ya msingi.
Alisema kwa sababu suala hili ni la kikanuni na Spika ameridhika kwamba
haki na maadili ya Bunge yamevunjwa, ni vizuri hoja ya Mbatia ijadiliwe.
“Mheshimiwa Spika, kwa vile ameridhika kwamba suala hili linahusu haki
na maadili ya Bunge, hatua inayofuata ni kuweka kipaumbele ili tujadili
hili suala. Hatujadili suala la kamati, wala kesi iliyoko Polisi,
tunajadili haya mengine yanayojitokeza ili hewa chafu inayojitokeza,
isafishwe,” alisema.
Akitoa mwongozo wake kuhusu hoja ya Mbatia, Spika Makinda alisema suala
hili lipo mikononi mwa Polisi na mtuhumiwa amekamatwa, hivyo uchunguzi
unaendelea.
Alisema kama ingekuwa halijapelekwa polisi, angelipeleka suala hili
kwenye kamati maadili na baadaye lingejadiliwa na Bunge lakini kwa vile
suala hilo liko Polisi, waachwe wafanye kazi yao.
Mnyika afichua siri
Akichangia bungeni kuhusu mswada wa sheria mbalimbali, Mbunge wa Ubungo,
John Mnyika (CHADEMA), alisema mtu aliyekamatwa akisambaza ripoti ya
CAG kama njugu, ana uhusiano na Waziri wa Nishati na Madini, Prof.
Sospeter Muhongo.
Alilitaka Bunge kuhakikisha inalibana jeshi la Polisi ili mtuhumiwa
achukuliwe hatua na kama ikithibitika kwamba ameiba nyaraka hizo kutoka
ofisini kwa Spika, atakabiliwa na adhabu ya kutupwa jela miaka mitatu.
Alisema tangu juzi mtuhumiwa huyo alipokamatwa, Polisi hawataki kumtaja
jina, wala uhusiano wake na Prof. Muhongo, lakini Ukawa wamefanya
uchunguzi na kubaini kuwa mtuhumiwa ni rafiki wa karibu na Muhongo,
wamesoma shule moja na amekuwa akija bungeni kila wakati wa mikuano ya
Bunge kwa ufadhili wa Muhongo.
Zitto Kabwe atungiwa kitabu kuchafua
Katika kipindi hiki cha kuelekea kujadili sakata la IPTL, hali katika
mji wa Dodoma sio shwari kutokana na matukio ya vitisho, watu kuchafuana
kiasi cha kushindwa hata kuaminiana.
Katika hali hiyo, Zitto ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), iliyopitia ripoti ya uchunguzi ya CAG kuhusu kashfa ya
Escrow Akaunti, ametungiwa kitabu kinachoeleza mambo mengi yakiwemo
madai yakuomba rushwa kutoka kwa mmoja wa wamiliki wa IPTL.
Kitabu hicho kimekuwa kikisambazwa kwa kutupiwa milangoni mwa nyumba za
wabunge na sehemu nyingine ili mradi nakala zake ziwafikie wabunge hao.
Mambo mengine yaliyomo kwenye kijarida hicho, yanahusu mambo binafsi ya
Zitto kama vile mahusiano ya kimapenzi na wasichana mbalimbali.
Kwa kifupi, kitabu hicho kimemchafua na kumuacha uchi Zitto, huku
akionekana kuwa sio mtu wa kuaminiwa kufanyakazi kama kiongozi wa PAC.
Zitto ajibu
Akizungumzia madai hayo, Zitto alihoji kuwa kwanini kitabu hicho
kimetungwa na kusambazwa sasa wakati anaongoza kamati nzito kuhusu
kashfa ya Escrow Akaunti.
Alisema lengo la watunzi wa kitabu hicho ni kutaka kubadili upepo wa
kashfa hiyo inayowasumbua baadhi ya vigogo nchini, ambao kwa sasa
hawapati usingizi.
“Mimi niwatake wabunge kujikita kwenye jambo moja kwa sasa la kashfa ya
Akaunti ya Escrow, mengine yote yanaweza kuja baadaye. Na niseme kama
kuna mtu ana hoja ya msingi kuhusu madai yaliyomo kwenye kitabu hicho,
afuate utaratibu wa kibunge, alete hoja bungeni ila kwa sasa akili zetu
zipo kwenye kukamilisha kazi tuliyoagizwa kuifanya,” alisema Zitto.
Hoja ya Mbatia
Mbatia jana alitoa hoja kutaka Bunge lisitishe shughuli zake ili
lijadili suala linalohusu haki za Bunge baada ya kubainika kwamba kuna
watu wameiba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kutoka ofisi ya Spika na kuzigawa kama njugu ili kupotosha ukweli.
Mbatia, alisema kwa mujibu wa kanuni ya 51 ya kanuni za Bunge toleo la
2013 analazimika kutoa hoja hiyo ili kujadili jambo hilo ambalo ni
muhimu kwa maslahi ya taifa.
Alisema kuwa siku ya Ijumaa 14 Novemba 2014 ofisi ya Spika ilipokea
taarifa ya Ukaguzi Maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kuhusiana na miamala iliyofanyika katika
Akaunti ya Escrow ya Tegeta pamoja na umiliki wa kampuni ya IPTL.
Alisema Novemba 17 mwaka huu siku ya Jumatatu, Naibu Spika alikabidhi
taarifa hiyo kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC)
ili ichambuliwe na baadaye iweze kuwasilishwa bungeni.
Kama ilivyokuwa kwa taarifa nyingine za ukaguzi maalum zinazotolewa na
CAG,taarifa hiyo ilikuwa ni ya siri na inatakiwa kuendelea kuwa hivyo
mpaka pale itakapowasilishwa bungeni.
Alisema jwa siku kadhaa wiki iliyopita wabunge kwa nyakati tofauti,
wamekuwa wakiomba taarifa hiyo iingizwe ndani ya Bunge na kuijadili
lakini wabunge tuliarifiwa kuwa kazi ya PAC haijakamilika na
itakapokamilika taarifa hiyo itawasilishwa.
“Katika hali ya kusikitisha wiki iliyopita min’ong’ono ikaanza kusambaa
katika mji wa Dodoma kwamba nakala ya taarifa hiyo zinagawiwa watu mjini
hapa kama njugu, baada ya kupata taarifa hizi mimi na baadhi ya
wenzangu wenzangu tulifanya jitihada za kufanya uchunguzi awali na
kuthibitisha minong’ono hiyo…
“Aidha tulimtaarifu Katibu wa Bunge ambaye kwa kushirikiana na jeshi la
polisi mkoani hapa walifanikiwa kumkamata mtu mmoja akiwa na nakala
nyingi za taarifa hizo, inasadikiwa kuwa mtu huyo anahusika katika
kudurufu na kusambaza taarifa husika na mpaka sasa ameshikiliwa na jeshi
la polisi.
Mbatia alisema kuwa inavyoonekana taarifa hiyo imeibwa baada ya
kupokelewa na Ofisi ya Spika kutokana na kuwa katika ukurasa wa Juu
kuna Muhuri unaosomeka kwa maneno meusi, “Ofisi ya katibu wa Bunge
imepokelewa 14 Novemba mwaka huu S.L.P 941 Dodoma”.
Kitendo cha taarifa hiyo kusambazwa mitaani wakati kamati ya PAC ikiwa
inaendelea na uchunguzi wake, kinamaanisha kuwa kuna watu wamejipanga
kuchafua heshima ya uongozi wa Bunge kwa kushusha hadhi na kuzuia Bunge
lisifanye kazi zake kama ifuatavyo….
“Kifungu cha 31(1) (g) cha sheria ya haki, kinga na Madaraka ya Bunge,
sura ya 296 kinamaanisha kuwa ni kosa la kwa mtu yoyote kusambaza
nyaraka yoyote inayoandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa Bungeni kabla ya
wakati.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment