Dodoma. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
amesema Kampuni ya Uwakili Mkono & Co. Advocates na Hunton &
Williams ya Marekani imejiingizia Sh62.9 bilioni kwa ajili ya kuendesha
kesi mbalimbali za Tanesco na IPTL hadi Septemba mwaka jana.
Profesa Muhongo aliyekuwa anatoa tamko la Serikali
dhidi ya Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ya
ufisadi wa Sh306 bilioni katika akaunti ya escrow, alilieleza Bunge jana
kuwa licha ya gharama, mawakili hao bado wanaidai Tanesco Dola za
Marekani 4.50 milioni (Sh7.8 bilioni).
“Kumalizika kwa mgogoro huu wa IPTL si tu kwamba
kumetuondoa kwenye hatari ya kuendelea kukamuliwa na mawakili hawa, bali
pia katika mazungumzo yaliyofanywa kati ya Tanesco na IPTL tumeweza
kuokoa takriban Sh95 bilioni katika madai ya awali ya IPTL,” alisema.
Kama fedha za escrow ni za umma
Profesa Muhongo alisema madai ya PAC kwamba fedha
zilizokuwa katika akaunti ya escrow zilikuwa za Serikali si ya kweli kwa
kuwa si za umma, bali fedha zote ni za IPTL.
“Huu si ukweli zipo sababu kuu zinazothibitisha kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema fedha zote zilizokuwa kwenye akaunti ya
escrow ni mali ya IPTL ambayo ikiwa wakala wa kodi inastahili kudaiwa na
kulipa kodi yoyote ambayo haijalipa.
“Kwa msingi huo, taarifa ya PAC haisemi ukweli
kuhusu fedha zilizowekwa katika akaunti ya escrow kuwa ni fedha za
umma,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema ili kuthibitisha kwamba fedha hizi siyo za
umma, CAG katika ukaguzi wake wa hesabu za Tanesco wa Desemba 31, 2012,
alielekeza kutoa fedha za escrow kwenye vitabu vya hesabu vya Tanesco
na kupunguza deni kwa kiasi hicho.
“Tanesco ina madeni na haijawahi kutengeneza fedha za umma,” alisema.
Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo alisema
madai ya PAC kuwa hapakuwahi kuwa na kamati ya uendeshaji kwa kipindi
chote cha mkataba wa PPA si ya kweli.
“Ukweli ni kwamba, kamati ya uendeshaji iliundwa
kabla ya kuanza uzalishaji wa mtambo mwaka 2002 na imeendelea kuwapo
hadi leo. Kamati hiyo ina wajumbe sita. Wajumbe watatu kati ya hao
wanatoka Tanesco na watatu waliobakia wanatoka IPTL,” alisema Profesa
Muhongo.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment