Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya
Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana
Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuomboleza vifo vya
Waandishi wa Habari, Innocent Munyuku wa Kampuni ya New Habari (2006)
Ltd. na Baraka Karashani ambaye alikuwa Mwanachama wa Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo nchini.
Mwandishi Mwandamizi, Innocent Munyuku alifariki akiwa usingizini
nyumbani kwake Kimara Jijini Dar es Salaam, wakati Baraka Karashani
aliaga dunia katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo Jijini Dar es Salaam
alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na vifo vya Waandishi hawa kwa
vile ni pigo siyo tu kwa Tasnia ya Habari waliyokuwa wanaitumikia na
Wanahabari kwa ujumla, bali pia kwa Taifa letu ambalo mchango wao kama
Waandishi wa habari ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu na Taifa kwa
ujumla”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais Kikwete amemwomba Dk. Fenella Mukangara kumfikishia Salamu zake
za pole kwa familia za Wanahabari hao kwa kupotelewa na mihimili na
nguzo muhimu za familia zao, lakini amewahakikishia wanafamilia kuwa
binafsi yuko pamoja nao katika kuomboleza misiba ya wapendwa wao.
“Namuomba Mwenyezi Mungu awape Wanafamilia wa Waandishi hao moyo wa
uvumilivu na subira kipindi hiki wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao,
na naomba azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za Marehemu,
Innocent Munyuku na Baraka Karashani, Amina,” amemalizia kusema Rais
Kikwete katika Salamu zake.
Post a Comment