RAIS KIKWETE AZINDUA UJENZI WA KITUO CHA MICHEZO YA VIJANA WADOGO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete amevitaka Vilabu vya mpira wa miguu nchini kuwekeza katika timu za vijana wadogo walio chini ya umri wa miaka 18 ili viweze kuwa na mafanikio ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo ameitoa  alipokuwa akizindua ujenzi wa kituo cha michezo cha vijana wadogo walio chini ya miaka 18 kinachojengwa nchini eneo la Kidongo Chekundu manispaa ya Ilala.
“Katika nchi yetu, timu ya soka ya taifa haifanyi vizuri na michezo mingine nayo
vivyo hivyo, vilabu mbalimbali vya michezo navyo havifanyi vizuri katika michezo yao
ya ndani na nje” alisema Kikwete.
Kikwete aliendelea kusema “Kiini cha timu yetu ya soka ya taifa na vilabu vyetu
kutokufanya vizuri katika mashindano, haviwekezi katika vijana wadogo”.
Katika kufanikisha adhima ya kuwa vilabu na timu ya taifa ya mpira wa miguu kuwa na mafanikio, Rais Kikwete amewaagiza viongozi Shirikisho la Mpira wa Miguu na wa vilabu vya mpira wa miguu nchini watekeleze majukumu yao ipasavyo ili soka la Tanzania liwe la mafanikio kwa wachezaji mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.





Aidha, amelishauri Shirikisho la mpira wa miguu nchini kuweka utaratibu ambao
utailazimu kila timu kuwa na timu ya vijana wadogo kama ilivyo katika mataifa mengine duniani ambapo kwa mataifa hayo, suala la kuwa na timu ya vijana wadogo na uwanja wao sio la hiyari.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Timu ya soka ya Sunderland ya nchini Uingereza ambao ndiyo watakaotoa wataalamu wa michezo watakaofundisha katika kituo hicho Bi. Margaret Byrne amesema kuwa kituo hicho kitakuwa na uwanja wa mpira wa miguu wa kisasa wenye ukubwa wa mita 100×60,viwanja viwili vya mpira wa kikapu, sehemu ya kuegesha magari 20 na kituo cha daladala, kiwanja cha kuchezea watoto.
 Bi. Margaretalisisitiza kwa ndani ya kituo hicho, kutakuwa pia na jengo la utawala,
vyumba vine vya wachezaji kubadilishia nguo vikiwa na vyoo na bafu, vyumba viwili vya wafanyakazi pamoja na chumba cha chakula ambacho kitaendana na madhari ya kituo hicho.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Symbion ya nchini Marekani Paul Hinks amesema kuwa kampuni yake iko mstari wa mbele nawataendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kukuza sekta ya michezo nchini kwa kujenga kituo cha soka kwa vijana wadogo.
Ujenzi huo ambao ulizunduliwa kwa kupanda mti wa mnazi unatarajiwa kukamilika mapema mwakani 2015 .
Source:Maelezo

Post a Comment

Previous Post Next Post