Mkurugenzi wa kituo cha huduma na sheria Zanzibar, Harusi Mpatani
Viongozi wa asasi hizo wakizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa jana, walisema janga la udhalilishaji wa kijinsia kwa kiasi kikubwa limepelekea waliotendewa ukatili kupata matatizo ya kiafya, kijamii, kiuchumi na kukwazwa kimaendeleo.
Walisema visiwani Zanzibar wanawake na watoto wanafanyiwa ukatili licha ya serikali kusaini mikataba ya kulinda haki za binadamu.
Mkurugenzi wa kituo cha huduma na sheria Zanzibar, Harusi Mpatani, alisema takwimu za hivi karibuni zinaonesha ongezeko kubwa la matukio ya kesi za ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto kufikia 2337 kutoka Juni 2013 hadi Julai, 2014.
Alisema kesi za watoto kutoka mwaka 2011 hadi 2012 zilikuwa 689 na mwaka 2013 hadi 2014 kesi 816 zilizoripotiwa katika wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto.
Alisema ukatili dhidi ya wanawake unaendelea unafumbiwa macho na kukubaliwa na baadhi ya watu hata taasisi za serikali.
“Hii siyo haki, ukimya umetawala kutoka katika taasisi za kiserikali na vyombo vya sheria,” walisema viongozi wa taasisi hizo ambazo za Zafela, Sos, Action Aid, Zapdd, Zlsc, Juwamaku na Save the New Generation.
Aidha, taasisi hizo zimesema katika kupambana na vitendo hivyo zimekuwapo changamoto mbalimbali ikiwamo ushirikiano mdogo kutoka katika jamii wakati wa kukusanya ushahidi.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment