Tamwa: Ukatili wa watoto waongezeka

Chama cha Waaandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa)
Chama cha Waaandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimevitaka vyombo vya usalama wa taifa, polisi na mahakama kushirikiana katika kupambana na wahalifu na wote wanaohusika katika kutekeleza vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa watoto nchini.
Tamwa imetoa kauli hiyo kufuatia idadi ya taarifa za ukatili na utekwaji wa watoto wa kike kuongezeka katika Dawati la Jinsia na watoto kwenye vituo vya polisi.

Taarifa ya Tamwa kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha Januari mpaka Septemba, 2014 idadi ya ukatili wa kijinsia kwa watoto kwa mkoa wa Dar es Salaam ni 519 hii ni pamoja na mikoa mitatu ya kipolisi yaani Kinondoni, Temeke na Ilala, ikifuatiwa na Zanzibar 219 (Unguja Magharibi na Kusini), Shinyanga 69, Mara 62, Tabora 55, Morogoro 36, Kagera 32 na mkoa wa Pwani 20.

“Katika taarifa za vitendo vya kikatili kwa watoto matukio yaliyojitokeza ni yale ambayo yanahusisha vitendo vya ubakaji, ulawiti, mateso, kutelekezwa kwa watoto, utekwaji nyara na kupotea kwa  watoto wa kike,” ilieleza.

Hivi karibuni mkoani wa Dar es Salaam zililipotiwa taarifa za watoto watatu waliokuwa wakisoma katika shule ya msingi Miembeni, huko Vingunguti waliopotea katika mazingira ya kutatanisha, taarifa ambazo zilitolewa na wananchi waishio maeneo ya Mbezi kwa Msuguri, Mbezi Msigani na vitendo vingine vya kikatili vimeripotiwa katika Wilaya ya Kinondoni na Temeke.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tamwa katika mradi wake wa Kujenga na Kuimarisha Usawa wa Kijinsia na Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia (GEWE II) kupitia Kituo chake cha Usuluhishi cha (CRC), kwa kipindi cha Oktoba mwaka huu kimepokea matukio 16 ya vitendo mbalimbali vya kikatili kwa watoto ambapo vimeongezeka kutoka matukio 9 ya Septemba.

Aidha, katika kipindi cha mwaka 2014 idadi ya matukio mpaka sasa imeongezeka kuwa 66 ikilinganishwa na ya mwaka 2013 ambapo taarifa za matukio zilikuwa ni 41.

“Tamwa inaamini kuwa vyombo vya usalama na sekta husika vikichukua hatua za makusudi na kuhakikisha wahalifu wanachukuliwa hatua za haraka kisheria kukomesha vitendo vya kikatili kwa watoto, taifa litaishi maisha yenye amani,” iliongeza
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post