MAMLAKA
ya usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imewashauri wawekezaji wa kampuni
za ndege hapa nchini kujiunga na kuanzisha kampuni moja ili kujitanua
katika soko la anga.
Ushauri huo ulitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo,
Charles Chacha, alipokutana na wawekezaji wa sekta hiyo wanaotoa huduma
katika idara mbalimbali ikiwemo chakula, usafirishaji mizigo na usafiri
wenyewe.
Chacha, alisema hiyo itawasaidia kuingia kwenye ushindani wa soko na
makampuni mengine ya nje kwa kuwa na ndege zenye kutoa huduma za viwango
vya kimataifa.
“Utakuta kampuni ina ndege moja na pale inapopata hitilafu safari
zinaahirishwa na hivyo kuleta usumbufu kwa abiria, lakini watakapojiunga
zaidi ya kampuni moja adha kama hizi zitaondoka na pia itasidia kupanua
mitaji yao,” alisema Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia kuhusu mkutano huo, alisema ni utaratibu ambao
wamejiwekea wakukutana na wawekezaji hao kila baada ya miezi mitatu,
lengo likiwa kupitia mabadiliko mbalimbali ya sheria, kuangalia
changamoto zinazowakabili na kubadilishna uzoefu wa kazi ambazo wamekuwa
wakizifanya kila siku.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Ndege, Laurence Paul, alisema bado
Tanzania haijatilia mkazo wa kutosha katika usafiri wa anga ikiwemo
kuunganishwa na sekta ya utalii.
Paul, alisema wakati sekta ya utalii inaongoza kwa kuliingizia fedha
taifa, suala la kuinganisha na usafiri wa anga haliepukiki kwa kuwa
watalii wengi wanatumia usafiri huo.
- Tanzania Daima
Post a Comment