
IDARA ya Uhamiaji inaanza msako wa nyumba kwa nyumba kubaini
wahamiaji haramu kwa kuchukua taarifa za wanandoa ambao wameolewa na
raia wa kigeni ili kubaini wahamiaji hao.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Kamishna wa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Grace Okororo, kwenye semina ya siku moja kwa Maafisa Watendaji
wa Mtaa wa Wilaya ya Ilala, iliyofanyika ukumbi wa Korea Jijini Dar es
Salaam.
Okororo alisema, kwa muda mrefu sasa wageni hususani wanaume kutoka
mataifa mbalimbali wamekuwa wakitumia mgongo wa kuoa wanawake wa
Tanzania ili kuweza kujipatia hifadhi.
Alisema wameamua kushirikiana na maafisa watendaji wa mitaa kutokana na kuwa karibu na wananchi.
“Kisheria mtu yoyote mgeni anayeingia nchini anatakiwa kutoa taarifa
kwa Mtendaji wa Mtaa lakini hilo kwa sasa halifanyiki jambo
linalochangia ongezeko la wahamiaji haramu wanaojihusisha na vitendo vya
uhalifu,” alisema.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhandisi Raymond Mushi,
alikiri kwamba watendaji wamekuwa hawalipi kipaumbele suala la wahamiaji
katika shughuli zao za kila siku.
Mushi alisema anaamini kwamba kila Mtendaji akitekeleza wajibu wake
ikiwemo kujitathimini kila siku ana imani suala la uhamiaji haramu
litapungua ama kuisha kabisa.
Aidha Naibu Kamishna Uhamiaji, Wilaya ya Ilala, Safina Muhindi alisema,
jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na wageni wengi kutokana na
kuwa kitovu cha shughuli mbalimbali ikiwemo biashara, shughuli za
kitalii, uwekezaji, diplomasia na masomo.
Post a Comment