Dar es Salaam. Kiwango cha kukubalika kwa utendaji kazi wa
baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini kimeshuka, ripoti ya utafiti ya
taasisi ya Twaweza iliyotolewa jana imesema.
Utafiti huo wa kisayansi uliwahusisha wahojiwa 1,445 wa Tanzania Bara ambao ulifanyika Septemba mwaka huu.
Mtafiti wa Twaweza, Elvis Mushi akitoa utafiti huo
unaoitwa Tanzania Kuelekea 2015 jijini hapa jana, alisema wananchi
walioulizwa walisema kiwango cha utendaji kazi wa makundi yote ya
uongozi kiko chini na kimekuwa kikishuka kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka
huu.
Alisema pamoja na utendaji wa Waziri Mkuu kuwa juu
kuliko wengine kitaifa, umeshuka kutoka asilimia 46 mwaka 2012 hadi
asilimia 32, mwaka huu.
“Kiwango kimeshuka zaidi hasa kwa wenyeviti wa
vijiji/mitaa na madiwani, ambapo kwa wenyeviti kimeshuka hadi asilimia
25 kutoka 54 mwaka 2012 na madiwani kutoka asilimia 44 iliyokuwa mwaka
2012 hadi 23,” alisema.
Kwa upande wa Rais, kiwango cha utendaji kimeshuka
kutoka asilimia 45 mwaka 2012 hadi 31 mwaka huu, Spika wa Bunge kutoka
asilimia 37 hadi 27 mwaka 2014, mbunge wa upinzani kutoka asilimia 33
hadi 18; mbunge kwa ujumla kutoka 40 mwaka 2012 hadi asilimia 24 mwaka
huu,” alisema Mushi.
Kwa mbunge wa CCM, utafiti huo umeonyesha kwamba utendaji umeshuka kutoka asilimia 25 hadi 15.
Katika utafiti huo, wananchi waliulizwa wanavyoona
kiwango cha utendaji kazi kwa ujumla wa viongozi mbalimbali wa kisiasa,
wa kuchaguliwa na wale wa kuteuliwa.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment