Wabunge wambana Katibu Mkuu Maliasii

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli
Wabunge wamembana Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Abelhem Meru, wakimtaka aisafishe Idara ya Misitu na Wanyamapori ya wizara hiyo kwa madai kwamba, ina matatizo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, alitoa agizo hilo katika kikao kati ya kamati yake na viongozi na watendaji wa wizara hiyo, wakiongozwa na Waziri wake,Lazaro Nyalandu, katika ofisi za Bunge, mjini hapa juzi.

“Katibu mkuu, uiangalie idara hii, kuanzia chini. Sisi tunawashauri.

Nyie ni watendaji. Sisi ni wanasiasa. Hatuna cha kupoteza. Idara ya misitu na wanyamapori ni shida,” alisema Lembeli. Alimtaka katibu mkuu huyo mpya kuziangalia taasisi hizo ili zifanye vizuri kama taasisi nyingine za wizara hiyo. Lembeli alisema itakapotokea idara inafanya vizuri, kamati yake haina hiana kupongeza.

Aliipongeza Mamlaka ya Hifadhi Nchini (Tanapa) na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)!kwa kufanya kazi vizuri.

Kauli hiyo iliyoungwa mkono na mjumbe wa kamati hiyo, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Suzan Kiwanga, aliyesema idara ya misitu imeshindwa kutunza maeneo iliyonayo nchini.

“Yaani mheshimiwa kule Katavi tulipoenda, miti imekatwa hadi imekwisha. Halafu unaambiwa ni eneo la misitu,” alisema Suzan. Kamati hiyo ilikataa kubariki marekebisho ya mipaka katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha (Anapa).

Marekebisho hayo yanatokana na mgogoro kati ya taasisi mbili za wizara hiyo; ambazo ni idara ya misitu na Tanapa.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post