
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
A;TUZO ZA WANAMICHEZO BORA 2013/2014
MIFUKO ya hifadhi ya Jamii ya NSSF na
PSPF imejitokeza kudhamini tuzo za Wanamichezo Bora wa Tanzania ambazo
zitafanyika Desemba 12 mwaka huu ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP), Dar es Salaam,
zikiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).
Udhamini wa PSPF katika tuzo hizo ni
Sh. Milioni tano, wakati NSSF imetoa Sh. Milioni mbili, hivyo kufanya fedha
taslimu ambazo hadi sasa TASWA imepata kufikia Sh. Milioni 37.
Wadhamini wengine ni Kampuni ya Said
Salim Bakhresa (SSB) Group Limited iliyotoa Sh. Milioni 10 na Kampuni ya Kufua
Umeme ya IPTL iliyotoa Sh milioni 20.
Uongozi wa TASWA unaendelea na mazungumzo na
kampuni mbalimbali kwa ajili ya kudhamini tuzo hizo, ambapo licha ya walioahidi
kutoa fedha taslimu, lakini wapo wengine tunaendelea kuzungumza nao kwa ajili
ya kudhamini kwa njia ya huduma zinazoambatana na tuzo hizo.
Ni imani ya TASWA kwamba hadi kufikia Novemba 20
mwaka huu kampuni na wadau mbalimbali walioahidi kutusaidia watakuwa
wametekeleza ahadi zao kulingana na mazungumzo tuliyofanya nao, hivyo
kuwatangaza rasmi.
Wanamichezo zaidi ya 100
wanatarajiwa kuwania tuzo kwa michezo mbalimbali, ambapo Kamati ya Tuzo za
Wanamichezo Bora wa TASWA, inatarajiwa kukutana wiki ijayo kujiridhisha kwa
mara ya mwisho orodha ya mapendekezo ya wanamichezo kutoka vyama mbalimbali vya
michezo kwa ajili ya kuwania tuzo hizo.
B; MEDIA DAY BONAZA
TASWA kila mwaka inaandaa bonanza la vyombo vya habari linalojulikana
kama Media Day Bonanza, ambalo hushirikisha wadau mbalimbali kutoka vyombo vya
habari.
Lengo la bonanza hilo
ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo,
uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya
habari, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Lakini
mwaka huu bonanza hilo limechelewa kutokana na na suala la wadhamini
ambao awali TASWA ilikubaliana nao, lakini baadaye walisema wamepata matatizo
ya kifedha.
Hata hivyo kutokana na umuhimu wa bonanza
hilo, uongozi wa TASWA umezungumza na wadau wengine na mazungumzo hayo
yanaendelea ili Media Day Bonanza ifanyike mwezi ujao likiwa ni maalum kwa
ajili ya kufunga mwaka 2014.
Tunajua maswali
kuhusu Media Day yamekuwa mengi pengine kuliko majibu, pia wasiwasi kwa baadhi
yenu ni mkubwa kuliko uhakika, lakini tunawahakikishia mambo yanaenda vizuri na
ni imani yetu yanakaribia kuiva.
Kwa hili la Media
Day, tuliona ni bora tukawie kuliko kuvurunda. Tusikimbie kwa kasi bila
kutazama tuendako. Tutambae, lakini macho njiani na mbele tunakoelekea na hiyo
ndiyo dhamira yetu.
Ahsanteni,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
07/11/2014
Post a Comment