Wahubiri wakataa juhudi za kuwalainisha

MWANASHERIA Mkuu, Githu Muigai (kushoto), Msajili Mkuu Bernice Gachegu (kati) na Kamishna Kamotho Waiganjo wa Tume ya Utekelezaji Katiba wakihutubia wanahabari baada ya kukutana na baadhi ya wahubiri jana. Picha/JENNIFER MUIRURI
VIONGOZI wa kidini jana walijiondoa kwa hamaki katika mkutano uliokuwa umeitishwa na Mkuu wa Sheria Githu Muigai kujadili mbinu za kulainisha shughuli zao.

Kundi lingine la viongozi waliokuwa wamealikwa lilisusia mkutano huo ambao Prof Muigai aliitisha kufuatia kisa cha majuzi ambapo Francis Kanyari wa dhehebu la Salvation Healing Ministry alianikwa hadharani kwa utapeli.

Miongoni mwa waliokosa kufika licha ya kualikwa ni Dkt Francis Kuria wa Baraza la Miungano wa Kidini nchini (IRCK), Padre KUTOKA UK 1 Vincent Wambugu wa Kongamano la Maaskofu Wakatoliki (KEC) na Kaasisi Peter Karanja, ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Makanisa nchini (NCCK). 
Badala yake waliandaa mkutano tofauti katika Jumba la Ufungamano walikoilaumu Serikali kwa kile walichosema ni kujaribu kusimamia pesa wanazopokea kutoka kwa waumini.

“Haifai kwa serikali kujaribu kudhibiti na kuingilia taasisi za kidini kwa kuanzisha kanuni mpya ambazo zinakinzana na uhuru wa kuabudu kama ilivyo katika Katiba,” akasema Askofu Mark Kariuki wa Muungano wa Wahubiri Nchini (EAK).

Alisema ni makundi ya kidini pekee yanayopaswa kudhibiti fedha yanazokusanya.

Kasisi Karanja alisema kuwa tukio la kanisa la Salvation Healing Ministry lake Bw Kanyari lilikuwa tofauti, na halipaswi kutumiwa kama kisingizio cha kuyaingilia makundi ya kidini.

Wengine waliohudhuria mkutano huo wa Ufungamani ni pamoja na Sheikh Adan Wachu (SUPKEM), Askofu David Oginde (kanisa la CITAM), Franklin Wariba (SDA), Bw Nitin Malde wa Baraza la Wahindu nchini miongoni mwa wengine Akiongea baada ya kukutana na viongozi waliobaki ukumbuni katika jumba la KICC, Prof Muigai alisema aliitisha mkutano huo kwa lengo la kuwashirikisha viongozi wote wa kidini kutathmini pendekezo la kubuniwa kwa mamlaka maalum ambayo itahusika katika usajili wa mashirika ya kidini.
- Taifa Leo

Post a Comment

Previous Post Next Post