Wananchi wamshukia Makinda, wabunge CCM

Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wamesema Spika Anne Makinda na baadhi ya wabunge wa CCM ndiyo chanzo cha Bunge hilo kusitishwa kwa dharura, kwani walionyesha wazi kuwabeba watuhumiwa waliotajwa katika ripoti zilizowasilishwa bungeni hapo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, walidai kuwa maelekezo waliyopewa na viongozi wao wa juu ya kuwatetea watuhumiwa ndiyo yaliyopelekea hali ya sintofahamu. Mkazi wa Tegeta, Jerome Tesha, alisema licha ya baadhi ya wabunge wa CCM kuonyesha msimamo wa kupinga hatua ya kuwabeba watuhumiwa lakini spika hakuliona hilo na kushikilia msimamo wake kwani aliamini kufanya hivyo ni kuingilia mhimili mwingine.
“Jana nilifuatilia kwa makini sakata hili, lakini hukumu yangu moja kwa moja naipeleka kwa Spika ambaye bila kupindisha maneno ndiye alikuwa kinara wa kuwabeba watuhumiwa hawa,” alisema Tesha.
Magreth Jonathan wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, alisema kutokana na ukiritimba uliokithiri miongoni mwa viongozi, wanashindwa kuchukuliana hatua wanapofanya makosa.
“ Huku kulindana kupita kiasi sijaona mantiki yoyote kwa Spika Makinda kuwabeba watu hawa ambao kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa bungeni zinaonyesha wazi wanahusika moja kwa moja na ufisadi huu,” alisema Jonathan.
Sweetbert Rwabukambara wa Mbezi wilayani Kinondoni alisema tabia ya wabunge wa CCM kulindana wameweza kumuambukiza hadi Spika wao ambaye juzi alionyesha dhahiri kulikingia kifua suala la watuhumiwa kuwajibishwa.
Akizungumzia suala la kukatika kwa umeme sehemu mbalimbali nchini wakati Bunge linaendelea, alisema alitarajia jambo hilo kutokea siku hiyo licha ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuagiza umeme usikatwe.
“Wakati Muhongo anawasilisha taarifa yake hawakukata umeme, lakini juzi wakati PAC wanafanya majumuisho umeme ulikatika, ” alisema Rwabukambara.
“Nilimsikia kwa makini sana spika ila lilipokuja suala la kuwawajibisha watu waliohusika alisema tunaingilia mhimili mwingine bila kutambua kuwa vitu hivi vipo wazi hata asiyesoma anaelewa,” alisema Joseph.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post