Mmh!
Haya sina jinsi kwa vile nimeamua kusema acha niseme, japo waswahili
wanasema pilipili usiyoilamba hujui kuwasha kwake. Lakini mtwanga
pilipili hakutaarifu ukohoe, hilo likae akilini. Leo jamani kidogo
nimeingia kwenye mavazi, najua mmeanza kunitazama kina dada wapendao
kutembea uchi.
Kwa kweli ifike hatua ujionee aibu kabla hujakosolewa na walimwengu,
unavaa nguo kama mkia wa mbuzi, haistiri mwili wala haikupendezi. Hivi
jamani huoni raha pale mpenzi wako anapokupapatikia baada ya kuondoa
nguo mwilini kwani alikuwa akiutamani ukiwa ndani ya nguo, vikiwa mezani
hamu inaongezeka mara dufu.
Mwanzo nilidhani ni sisi wakina sina mume ndiyo huvaa mavazi ya
mitego ili angalau tukikosa papa basi tupate dagaa mchele. Lakini kumbe
sivyo, wengine wake za watu na mumewe anatazama kesho ukisikia katembea
na mkata majani unakuja juu. Nani alikuambia mbuzi anajichunga
mwenyewe.
Huu utandawazi umewafanya wanaume wengi kuwa mazezeta, jamani wazazi
wetu ndivyo walivyotulea? Mtoto wa kike enzi zetu ulikuwa huoni matiti
wala mapaja, nguo ya ndani ndiyo usiseme, shangaa mamaaaa utazionea
wapi.
Ilikuwa aibu kubwa kwa mtoto wa kike kuonesha vitu hivyo, lakini leo
mwanamke kageuka mbuzi, kutembea uchi wala hajali. Watoto wa kike tokea
ndani ya nyumba zao wanakaa uchi eti kwenda na wakati. Jamani tunakwenda
wapi mbona tunapotea?
Sasa hivi wasichana wanavaa nguo fupi nguo za ndani nje shanga ndiyo
usiseme. Sasa hivi changudoa hajulikani na mke wa mtu vilevile, wote
mwendo huohuo. Mnajua nini hili nalisema bila hofu sikuogopi japo
litakukera. Sisi wanawake tuna akili za kushikiwa kila kitokacho lazima
tukifanye, ukija mtindo wa kuvaa magunia wote tunavaa ili mradi
tusipitwe na wakati.
Kwa vile hatutaki kupitwa na vitu hata wanawake walio ndani ya ndoa
wanaona machangudoa au wakosa haya kutembea uchi wanakwenda na wakati
nao wanayafanya hayo. Aiii jamani, nataka kuwaeleza kitu kimoja ndoa ni
zaidi ya kupiga goti kwenye madhabahu.
Mungu anaitambua ndoa, ndiyo maana huwakusanya watu kuishuhudia
wakiwepo viongozi wa dini. Tukiambiwa tuna akili ya mbuzi
tusikasirike.Jamani tuheshimu mavazi, utu wetu matendo huonekana kwa
macho ya moyoni ni siri ya mtu. Huwezi kusema tabia yangu nzuri wakati
unatembea uchi.
Tujistiri basi, ili tudumishe heshima ya mwanadamu, tujitofautishe na
wanyama.Sasa hivi tumekuwa wanyama, kutembea uchi na kufanya mambo ya
aibu bila kuona haya.Hata kuaga nimesahau mnaniudhi ati, tukutane wiki
ijayo. Anti yenu Nasra Shangingi Mstaafu.
Post a Comment