
Inaelezwa kuwa hali hiyo inatokana na kupanda kwa
gharama za maisha pamoja na umaskini uliokitihiri kwa baadhi ya familia
zinazoishi jirani na machimbo ya wachimbaji wadogo wa dhahabu wilayani
Geita.
Hatua hiyo inadaiwa kukiuka agizo la Serikali la kuzuia watoto kuonekana kwenye machimbo au kutumikishwa kwenye shughuli hizo.
Watoto wanaodaiwa kuathirika zaidi na shughuli
hizo ni watoto wadogo wanaonyonyeshwa, ambao huambatana na wazazi wao
wanaotegemea kipato cha familia kwa kuponda mawe katika machimbo hayo.
Mwananchi limeshuhudia baadhi ya wanawake katika
machimbo ya Nyarugusu wilayani Geita wakifanya kazi hizo, huku wakiwa na
watoto wao mgongoni bila kujali maradhi yanayoweza kuwapata watoto wao.
Wachimbaji wadogo hutumia zaidi maji
yaliyochanganywa na kemikali ya zebaki kuosha mchanga wenye madini ya
dhahabu ambayo hata hivyo hutiririka kwenda kwenye vyanzo vya maji.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita,
Dk Adamu Sijaona alisema kwamba maradhi yanayoweza kutokea kutokana na
kemikali hizo ni magonjwa ya ini.
‘’Kemikali hizi ni hatari sana kwa afya za watu,
kwani kama mtu akivuta hewa inayotokana na kemikali hizi anaweza kupata
ugonjwa wa ini ambalo linaweza kuharibika,’’ alisema Dk Sijaona.
Baadhi ya wanawake waliozungumza na gazeti hili
kuhusu kujishughulisha na ujira huo na wakiwa na watoto wao mgongoni
walisema wanafanya hivyo kutokana na kukosa wasaidizi wa kukaa na watoto
nyumbani.
Pia, walisema umaskini unaozikabili familia zao
unasababisha wao kwenda kutafuta kazi katika machimbo hayo ili kulisha
familia zao na kujipatia fedha za kuwasomesha watoto wao.
‘’Sina mtu wa kumwachia mtoto...Watoto wangu
wakubwa wameenda shule...kwa hiyo nitamuacha na nani sasa...Nikisema
nikae nyumbani wanangu watakula nini, shughuli hizi zinatusaidia
kusomesha watoto, tunakula kutokana na kazi hizi,’’ alisema Sophgia
Thomas.
Walisema hulipwa Sh5,000 kwa mfuko mmoja na kwa siku mtu mmoja ana uwezo wa kuponda mifuko mitatu hadi mine ya mawe.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment