2,672 waambulia sifuri kidato cha nne Lindi

Mkuu wa mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula.
Wanafunzi wapatao 2,672 kati ya 4,425 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha  nne kitaifa mwaka huu mkoani hapa, wamefanya vibaya katika matokeo yao kwa kupata alama sefuri.
Takwimu hizo zimetolewa na mkuu wa mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula wakati akikabidhi ofisi na majukumu mengine kwa mkuu mpya wa mkoa wa Lindi, Mwantumu Bakari Mahiza hivi karibuni.

Magalula alisema wanafunzi wapatao 1,753 ndiyo waliojitahidi kufanya vizuri kiasi, kwa mujibu wa matokeo hayo.

Alifafanua kuwa wanafunzi 19 kati ya hao waliosajiliwa kufanya mtihani huo, walipata alama ya daraja la kwanza, 118 daraja la pili,  326 daraja la tatu na 290 daraja la nne.

Alisema kiwango cha elimu kitaifa, kuanzia shule za msingi hadi sekondari katika mkoa huo wa Lindi, bado kipo cha chini ikilinganishwa na mikoa mingine nchini.

Kwa upande wa elimu ya msingi, Magalula ambaye kahamishiwa mkoani Tanga kuendelea na wadhifa huo, alisema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2012 kilikuwa ni asilimia 22.26 wakati mwaka 2013 ni asilimia 41.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea Mahiza, wakiwemo viongozi wa dini,vyama vya siasa na wakuu wa Idara za Serikali  baada ya kukabidhiwa ofisi yake mpya, ameomba kupewa ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kuleta maendeleo kwa jamii.

Mahiza aliomba apate muda wa mwezi mmoja kuutembelea mkoa wake mpya ili kufahamu changamoto zilizopo kabla hajaanza kupanga mikakati yake.

“Nina shukuru kwa mapokezi mazuri mliyonipatia, lakini ninachopenda kuwaomba nipate muda kidogo japo mwezi mmoja niweze kutembelea mkoa wote na baada ya hapo ndipo nifahamu pa kuanzia, ”alisisitiza.

 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post