
BIWI
la simanzi lilitanda katika mtaa wa Mutirithia, mjini Molo baada ya
mwanamume mwenye umri wa makamo kumpiga mwanawe hadi kufa kwa madai ya
kula andazi maarufu kama kangumu bila ruhusa.
Kulingana
na jirani yake, Bw Stephen Ngugi, jamaa huyo ambaye ni mlevi kupindukia
alifika nyumbani kwake majira ya usiku na baada ya kuarifiwa kwamba
mtoto huyo alikula andazi ili kupunguza makali ya njaa, alimpiga hadi
akazirai kabla ya kumgonga kichwani kwa kutumia stuli, pigo ambalo
lilipelekea mtoto kuvuja damu nyingi.
“Nimemjua
mtu huyu kwa zaidi ya miaka kumi na amekuwa mlevi kupindukia. Na
niliposikia mayowe nyumbani kwake nikafikiria pengine ashalowa maji ndio
maana kapiga kelele,” Ngugi alisema. Ngugi alielezea kuwa jamaa huyo
vile vile huvuta bangi na kwamba huenda ndio chanzo cha kutekeleza
mauaji hayo. Bi Phylis Wangui ambaye ni shangazi ya watoto hao alisema
mtoto huyo, ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya
wavulana ya Mt Mary’s mjini Molo amekuwa mtiifu hata ingawa babake
amekuwa akiwatesa haswa baada ya kutalakiana na mama yao. Aidha, Bi
Wangui alielezea Taifa Leo kwamba baada ya jamaa huyo kutekeleza mauaji
hayo ya kikatili, alizitupa baadhi ya nguo alizovaa mtoto huyo na ambazo
zilikuwa zimelowa damu kwenye choo ili kuficha ushahidi wa unyama
aliomtendea mwanawe. Hata hivyo, jamaa alisahau kulikuwa na alama za
damu zilizotapakaa kila mahali, na hata kwenye ukuta na pia kwenye
godoro. Wangui amesema baba huyo mlevi na ambaye pia hutumia bangi
wamekuwa wakizozana mara kwa mara na mkewe kabla ya kutalakiana kwa muda
wa miezi mitatu kwa sasa. Hatua za kisheria Bw Sammy Karanja, ambaye ni
babuye marehemu ameitaka serikali kumchukulia hatua za kisheria
mshukiwa na pia kuwapa ushauri nasaha watoto wawili ambao walishuhudia
baba yao akimtendea ukatili ndugu yao. “Nina huzuni tele kufuatia kifo
cha kijana huyu mdogo na ningeomba hatua za kisheria zichukuliwe dhidi
ya mshukiwa,” alisema babu huyo. Wakazi wa mtaa huo wameelezea kusitika
kwao kufuatia mauaji hayo ya kikatili huku wengi wakitiririkwa na
machozi kuona maovu na uhayawani ambao umetekelezwa na baba dhidi ya
mwanawe. Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia
maiti cha hospitali ya Molo huku mshukiwa akiwa katika kituo cha polisi
akisubiri kufunguliwa mashtaka
Post a Comment