‘Changa la macho’ hadi kwa wachezaji!

Nakumbukuka sehemu ya hotuba moja ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema kuna zuzu kauziwa almasi feki halafu anaondoka, alikuwa na almasi akadanganywa akaambiwa, almasi siyo hii, almasi ni hii. Kumbe ni chupa.
Ndiyo maana nimeanza hivyo kwa kumnukuu Nyerere ambaye alikuwa akiona mbali sana katika kauli zake.
Juzi nilimsikia kocha mkuu wa Yanga, Marcio Maximo akiwaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa waondoe hofu kwani kiungo mkabaji mpya aliyekuja naye kutoka Brazil, Emerson De Oliveira Neves Rouqe ni kifaa na ana uwezo wa kucheza popote.
Maximo aliwasili Dar es Salaam katikati ya wiki iliyopita akiambatana na Emerson na kupokelewa na mashabiki wa Yanga.
Mara baada ya kuwasili, Maximo alisema hana hofu na mchezaji aliyekuja naye kwani ni aina ya wachezaji wanaobadilika ndani ya uwanja kulingana na aina ya mchezo. Kauli kama hiyo ya Maximo aliitoa Julai 15, 2014 baada ya kuwasili kwa Geilson Santos Santana ‘Jaja’ wakati huo akitokea Sao Paul.
Jaja ambaye alikuwa akichezea timu ya Itabaina FC nchini Brazil, alikuwa mchezaji wa pili kuungana na kikosi cha Yanga baada ya Andrey Coutinho kuwasili.
Maximo alipamba kauli zake kama ilivyokuwa kwa Jaja na juzi wakati Emerson anaingia alisema: “Mashabiki wa Yanga hawatajutia ujio wa Emerson kwani ni mchezaji wa kimataifa, amecheza soka nchi nyingi, ndani ya uwanjani anajua nini anafanya, ana uwezo wa kubadilika kulingana na mchezo.”
Nakumbuka Maximo aliyempamba Jaja kabla ya kukubali aondoke baada ya kuchemsha, juzi alirejea kumpamba, Emerson kuwa ana uwezo wa kubadilika na kuendana na mpira.
Katika kujitetea suala la Jaja, Maximo alisema kwa kifupi “Jaja aliondoka kwenda Brazil na huko amepata matatizo ya kifamilia, lakini hajapata bado barua rasmi kama ameachwa, siwezi kulizungumzia sana hilo kwani bado anasubiri barua rasmi kutoka kwa viongozi.” Hapa ni ‘fiksi’ tu ni kwamba katemwa.
Nilifikiria mengi baada ya Jaja kuondoka, nilifikiria mengi baada ya Emerson kuja nikiwaza tunakosea kuingia mikataba mbalimbali, jamani hata kwa wachezaji tunabugi?
Hivi Kamati ya Ufundi ya Yanga, inamfahamu vizuri huyu Emerson? Wakati Jaja analetwa hadi kuvuma na leo anaonekana si lolote, ni kwamba hakukuwa na mtu anayemfahamu. Hata wewe unayesoma hapa, ukipata dili la kufundisha popote hasa nje, ni wazi utaondoka na mtu wako tu na ndivyo alivyofanya Maximo. Nani kati yenu Yanga anamjua vizuri Emerson?
Ni wazi na ninaamini hivyo, Emerson atavuna dola zake na kuondoka. Tunakosea mikataba mbalimbali ya madini, uwindaji, uvunaji magogo na hata kwa wachezaji? Hao wamekuja kuitia klabu hasara tu wakati kuna wachezaji wazuri Tanzania ambao hawajapewa nafasi.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post