Dk Karl Peters alizaliwa mwaka 1856 akiwa mtoto wa nane wa mchungaji wa Kilutheri. Baada ya masomo ya sekondari alisoma historia na falsafa katika vyuo vikuu vya Gottingen, Tubingen na Berlin alipohitimu shahada yake ya uzamivu.
Kwa muda wote aliokuwa chuoni, alivutiwa zaidi na
falsafa ya Udarwini wa Kijamii ambao moja ya mafundisho yake ni kutoa
haki kwa wenye nguvu na wababe duniani kuwatawala na kuwakandamiza watu
dhaifu.
Mafundisho haya kwa kiasi kikubwa yaliathiri tabia yake na kumuondolea roho ya ubinadamu.
Suala la Ujerumani kutokuwa na koloni hadi muda
ule lilimsikitisha na aliamini kuwa Ujerumani kama taifa kubwa barani
Ulaya, ilistahili kuwa na makoloni mengi kama ilivyokuwa Uingereza.
Mnamo Machi 1884 alianzisha Shirika la Ukoloni wa
Kijerumani. Baada ya hapo aliandaa safari yake ya Afrika kipindi ambacho
mataifa ya Ulaya yalikuwa yakiandaa mkutano wa Berlin kuhusu makoloni.
Alipofika Afrika Mashariki baada ya kupata idhini
kutoka kwa Sultani wa Zanzibar, aliingia mikataba ya kilaghai na machifu
wa Usagara, Uzigua, Nguru na Ukami na katika muda mfupi, yaani kuanzia
tarehe 23 Novemba hadi 17 Desemba 1884, alijipatia jumla ya eneo la
kilometa 140,000 za mraba.
Mwanzoni Serikali ya Ujerumani haikumuunga mkono,
lakini baadaye iliridhia na akafanikiwa kuanzisha koloni la Wajerumani
la Afrika Mashariki.
Wanahistoria wengi wanamkumbuka Karl Peters kama
mtu katili,m asiyekuwa na hata chembe ya ubinadamu. Alijijengea umaarufu
mkubwa miongoni mwa wenyeji hasa kutokana na matendo yake ya ukatili
dhidi ya wananchi.
Kutokana na ukatili wake wananchi wakambatiza jina
la Mkono wa Damu. Alifanya maovu mengi ambayo kama ingekuwa katika zama
tulizonazo pengine angeburutwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu
(ICC).
Mwaka 1891, akiwa na cheo cha kamishna wa Kaisari
katika eneo la Kilimanjaro, alifanya kituko kimoja ambacho ni mfano
mbaya kabisa wa matumizi mabaya ya madaraka.
Akiwa kiongozi alikuwa na tabia ya kuwa na mabinti
wengi wenyeji aliowatumia kama wapenzi wake. Usiku wa tarehe 18 Oktoba
1891 alimfumania mmoja kati ya wapenzi aitwaye Yagodja akiwa na mtumishi
wake wa kiume aitwaye Mabruk.
Akiwa na hasira kali, mara moja Peters akaitisha
mahakama ya kijeshi akiwa yeye mwenyewe hakimu na kumhukumu Mabruk
anyongwe hadi afe. Yagodja alikimbia lakini alikamatwa mnamo Januari
1892 akahukumiwa adhabu ya viboko na kunyongwa hadi afe. Haikuishia
hapo, akaamuru kijiji alichotoka Yagodja katika eneo la Rombo kichomwe
moto. Ilipofika hapo Wachagga hawakukubali. Walinyanyua juu silaha zao
na kupambana na Wajerumani. Kama si ujasiri wa Kapteni Emmil von
Wissmann Wajerumani wangeng’olewa eneo la Kilimanjaro.
Post a Comment