Jaji Warioba aunguruma Mwanza, ataka majibu ya hoja zake

Mwanza. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba amesema licha ya kushambuliwa kwa mambo ya msingi anayozungumza kuhusu Katiba Mpya hakuna mtu aliyejitokeza kumjibu hoja zake, zaidi kumpiga vita.
Aidha katika mdahalo huo  Mkurugenzi wa Taasisi Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema kamwe mtu huwezi kutengeneza Katiba kama nimuongo, mnafiki na mtu mbinafsi.
Akizungumza kwenye mdahalo huyo uliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Gold Crest mkoani mwanza huku akisikilizwa na mamia ya watu waliojitokeza eneo la tukio, Jaji Warioba amesema siku zote hoja nzito haziwezi kujibiwa kwa majibu mepesi.
Amesema kama Tanzania inataka kupata katiba nzuri na itakayodumu kwa muda mrefu hekima, uwezo na uadilifu vinaweza kuwa vigezo vya watungaji wa katiba hiyo na wala  hatuwezi kuipata kwa lugha za matusi na kejeri.
Jaji Warioba anasema, “Mimi nimekuwa nikizungumza mambo ya msingi kuhusu Katiba iliyopendekezwa, lakini hakuna anaejitokeza na kunijibu, zaidi ya kunijibu kwa mambo mengine wanayoyajua wao.”
Anaongeza, “Katika majibu yao makubwa utawasikia wanasema mimi nimemsaliti Mwalimu Nyerere, kuna baadhi ya mambo ninayoyasema hata Mwalimu Nyerere angekuja leo angeniunga mkono."
Warioba anasema wao walipendekeza mambo mengi kuhusu maadili kwenye Katiba iliyopendekezwa, lakini Bunge Maalumu la Katiba liliyaondoa na kubakiza mamchache, huku wakieleza kwamba mengine yatatungiwa sheria.
Warioba anasema mbali na hilo Mwalimu  Nyerere aliwahi kupitisha ajenda kwamba Wabunge wakae kwenye majimbo yao, Je, angeurudi  leo na wananchi wakamueleza  jinsi hali ilivyo tunazani angekubaliana na jambo hilo, hivyo kwa taifa lolote maadili ya viongozi ni kitu cha msingi.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku anasema kwa sasa wao wanafanya kazi ya kuwaelimisha wananchi nini maana ya Katiba, kwani Katiba ni sheria mama kwenye nchi ya watu wastarabu.
“Huwezi kutengeneza Katiba kama wewe ni muoga, mnafiki unayetaka Kutengeneza Katiba kwa ajili ya tumbo lako. Naomba wananchi elimu hii tunayowapa isiishie hapa mkitoka kwenye mdahalo huu huko mitaani vijiweni nendeni mkazungumze,”anasema Butiku.

Post a Comment

Previous Post Next Post