JK kumaliza hamu ya Watanzania Jumatatu?...

Rais Kikwete.
Hamu ya Watanzania wengi waliokuwa wakisubiri maamuzi kuhusu watuhumiwa wa sakata la akaunti ya Escrow huenda ikamalizika Jumatatu wakati Rais Jakaya Kikwete, atakapozungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Gurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu jana, kwa vyombo vya habari ilisema kuwa Rais Kikwete, anatarajiwa kuzungumzia masuala mbali mbali ya kitaifa, yakiwemo yale ambayo yamekuwa yanasubiri maamuzi yake tokea alipokuwa anajiuguza baada ya upasuaji aliofanyiwa mwezi Novemba.

Awali ilifahamika kuwa Rais Kikwete angezumza na wazee hao jana, taarifa ambazo zilikanushwa na Ikulu.

"Rais Kikwete atazungumzia masuala mbali mbali ya kitaifa, yakiwemo yale ambayo yamekuwa yanasubiri maamuzi yake tokea alipokuwa anajiuguza kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita," ilisema taarifa hiyo.

Watanzania wengi wamekuwa wakisubiri maamuzi ya Rais, baada ya Bunge kupitisha maazimio yake kuhusu watuhumiwa wa sakata la akaunti hiyo.
Tayari aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, amejiuzulu  wadhifa wake, kwa kuandika barua mapema wiki hii kwa kueleza kuwa ushauri wake kuhusu akaunti hiyo haukueleweka.

Wengine wanaotuhumiwa kuhusika na sakata hilo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.

Katika mjadala uliohusu sakata hilo, Bunge lilitoa mapendekezo ya maazimio likiwemo la Rais kuwawajibisha.

Wakati sakati hilo likijadiliwa bungeni, Rais Kikwete alikuwa nchini Marekani kwa matibabu ya upasuaji.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post