Mbunge huyo kijana, ndiye aliyeibua sakata hilo
wakati wa Bunge la Bajeti akituhumu kuwapo kwa wizi wa zaidi ya Sh200
bilioni zilizowekwa kwenye akaunti hiyo iliyofunguliwa Benki Kuu ya
Tanzania, kutunza fedha ambazo Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)
lilitakiwa liilipe Kampuni ya ufuaji umeme ya IPTL kusubiri uamuzi wa
mahakama kuhusu kesi iliyofunguliwa na Tanesco kupinga viwango vya tozo
hiyo.
Hoja hiyo ilijadiliwa kwa siku tatu na Bunge na
baada ya mjadala mkali, Jumamosi Bunge lilifikia maazimio ya kutaka
waliohusika wote, ambao ni wanasiasa, wafanyabiashara, waajiriwa kwenye
ofisi za umma na taasisi zilizohusika za fedha, kuchukuliwa hatua kwa
mujibu wa sheria.
Baada ya kuwasilisha hoja hiyo Mei 8, mwaka huu
akihusisha mawaziri wawili, Kafulila alilalamika bungeni kuwa anatishiwa
maisha, lakini alionekana kutotetereka hadi Bunge lilipofikia uamuzi
Jumamosi.
“Mambo manne yaliyonipa ujasiri wa kulisimamia
hili na kuona kuwa hatua zinachukuliwa ni pamoja na Mosi, utata wa kifo
cha waziri wa zamani wa Fedha, Dk William Mgimwa,” alisema mbunge huyo
kutoka NCCR-Mageuzi akiongeza kuwa kifo hicho kilimshtua na mazingira
yake yalikuwa na utata kiasi cha kuona kuwa kuna haja ya kukomalia
sakata la escrow.
“Baada ya kifo chake, kichwa kilini-click, nikajua
tu hapa kuna kitu. Sikutaka kuishia hapa. Kuna kifo cha meneja biashara
wa petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius
Gashaza ambaye alijiua baada ya kutoka Dodoma… kuna utata utata hapa,”
aliongeza Kafulila.
Ofisa huyo wa Ewura alijiua kwa kujinyonga siku
moja akiwa kwenye nyumba ya wageni jijini Dar e Salaam baada ya kutoka
Dodoma ambako aliitwa kuhojiwa kuhusu kodi za mafuta na makusanyo yake.
“Pili, nilikomalia hili kwa kuwa nilikuwa nina
nyaraka 604 za (transactions) za TRA kulalamikia kutolipwa fedha zake za
kodi, barua za kutoka na kwenda Hazina, BoT, Benki za Stanbic,
Mkombozi, kwenda kwa wahusika wote waliokumbwa na kashfa ya escrow na
ndiyo maana sikuwa na hofu hata kidogo.
“Tatu, ushahidi wa mauziano ya hisa kwa Kampuni ya
Mechmar (iliyokuwa inamiliki hisa za IPTL) kwenda kwa Kampuni ya
Piperlink Limited ya British Virgin Island na mengine mengi na nne,
nilikuwa ninajiamini kwa kuwa nilikuwa na barua ya TRA iliyokuwa
ikilalamikia kutolipwa kwa kodi ya ongezeko la thamani baada ya
kufanyika kwa miamala mbalimbali.”
Kafulila (32), ambaye alidokeza kuwa anataka
kutunga kitabu kuzungumzia suala la escrow, alidai kuwa alipata vikwazo
vingi kwani wabunge wengi walidhani anafanya mzaha na ndiyo maana
wakampuuza, lakini anasema alisimamia alichokiamini.
“Nimejifunza mengi katika hili, mwanzoni
nilipuuzwa niliambiwa tena na (Waziri wa Nishati na Madini,) Profesa
(Sospeter) Muhongo kuwa ninataka kuichonganisha Serikali, nina nyaraka
za uongo na hakuna uhakika wa ninachokisema na kwamba ninatumiwa,”
alisema Kafulila.
“Waliniambia ninatumiwa na IPTL kuichafua
Serikali. Niliambiwa ninatumiwa na (Mwenyekiti wa Kampuni za IPP,)
Reginald Mengi- huyo Mengi sijawahi kukaa naye hivi- kummaliza Profesa
Muhongo, na wapo waliosema ninatumiwa na Mbunge wa Musoma Vijijini,
Nimrod Mkono kuchafua wengine. Yapo mengi yamesemwa, lakini
sikutetereka.”
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment