HUKU moto wa upotevu wa
fedha za umma katika akaunti ya Tegeta Escrow ukiwa bado unawaka
kufuatia mawaziri wawili, mwanasheria mkuu wa serikali, katibu mkuu
mmoja na Bodi ya Tanesco kutakiwa kuwajibishwa, mali zinazomilikiwa na
vigogo waliochotewa fedha hizo usipime.
Moja ya ghorofa la kifahari katika maghorofa yanayomilikiwa na vigogo wa Escrow.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa wanaotajwa kunufaika na fedha
hizo, unaonyesha kuwa, pamoja na mambo mengine, wanamiliki majumba
makubwa ya kifahari, yakiwemo maghorofa katika maeneo mbalimbali ya
mikoa, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Morogoro.
Mmoja wa wanaotajwa (jina linahifadhiwa kwa sasa) ana jumba kubwa la
ghorofa mbili sehemu za Mbezi Beach, Dar, ambalo licha ya kuwa ya
thamani kubwa, pia ukubwa wa eneo analomiliki, umemfanya pia kujenga
bwawa kubwa la kuogelea.
“Aina ya maisha anayoishi huwezi kusema kama ni Mtanzania, kwa sababu
haonyeshi kama anajua uwepo wa shida, kwa sababu watoto wake wote
wanasoma nje ya nchi na zipo likizo ambazo hawarudi kwa vile wanasafiri
nchi tofauti na wanazosoma kwa ajili ya matembezi tu.
“Acha hii nyumba, ana ghorofa pale Kariakoo
lote limepangishwa na magari anayoendesha huyu bwana ni hatari.
Nafikiri gari la thamani ndogo kabisa ni BMW analoendesha mkewe. Kuna
watu wana fedha hadi wanaudhi aiseee,” alisema mkazi mmoja wa Mbezi
Beach, anayedai kuishi jirani na mfanyabiashara huyo aliyenufaika na
fedha za Escrow.
Muonekano wa juu wa ghorofa hiyo.
Kigogo mwingine mwenye asili ya Mwanza, anadaiwa kununua jengo lenye
ghorofa nne lililopo katikati ya Jiji la Mwanza na limeshaanza kufanyiwa
marekebisho, kwani ana lengo la kuifanya hoteli.
Wakati ikiwa bado haijafahamika kama watu hao walionufaika na fedha
hizo mali zao watafilisiwa au la, habari zinasema baadhi ya
waliochotewa, wamekuwa na maisha ya kufuru, kutokana na matumizi ya
kutisha ya fedha wanayofanya, huku wakinunua vitu mbalimbali vya
thamani.
Hata hivyo, wakati watu hao wachache wakiwa wamegawana kiasi cha
shilingi bilioni 306, idadi kubwa ya Watanzania wanaishi maisha ya
umaskini mkubwa, kiasi cha kula mlo mmoja kwa siku, huku wakikosa huduma
muhimu kama maji safi na salama ya kunywa, huduma bora za afya na
elimu.
Mamia ya vituo vya afya vinavyomilikiwa na
serikali huko vijijini havina dawa, hasa kipindi hiki ambacho serikali
inadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 90 na Bohari Kuu ya Madawa (MSD).
Kutokana na kukosekana kwa dawa, Watanzania wengi hufariki dunia kwani
zahanati nyingi zina dawa ndogondogo kama panado za kutuliza maumivu tu.
Muonekano wa ndani wa ghorofa hiyo.
“Wakati wengine wanakufa kwa kukosa dawa, shule zikiwa hazina vifaa
vya kufundishia na uhakika wa kula ukiwa mdogo, Watanzania wengine
wanaishi kifalme, wanapata kila kitu wanachotaka, wanakwenda popote
wanapotaka, wanatibiwa hospitali wanazotaka. Bora maisha wanayoishi
yangekuwa kwa sababu ya fedha halali, lakini hizi za wizi ni hatari
sana,” alisema mwanaharakati mmoja, aliyejitaja kwa jina moja la Nando.
Wiki iliyopita, Bunge lilitoa maazimio nane yanayotakiwa kutekelezwa
na serikali, ikiwa ni pamoja na kupendekeza mamlaka ya uteuzi kuwavua
nyadhifa zao Mawaziri Sospeter Muhongo na Anna Tibaijuka, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini,
Eliakim Maswi pamoja na kuvunjwa kwa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme
(Tanesco).
Bunge hilo pia, lilimjadili Singasinga Harbinder Sigh Seth (pichani) ambaye inadaiwa ndiye kinara wa dili hilo.
CREDIT: UWAZI
Post a Comment