MARASHI MAZURI YAMESABABISHA WENGI KUIBIWA

https://encrypted-tbn2.gstatic.com/images?q=tbn:ANd9GcQdsicqaHmj0j0buzKpl5uPjY2lT8yfIyr4v_ui_EAuwsT0vAwZbA
HIVI sasa kuna kundi la matapeli lenye mchanganyiko wa wanaume na wanawake ambao hutumia ujanja wa kujifanya wana marashi mazuri, kisha huwatapeli watu.
Matapeli hao hujifanya ni watu wa ngazi za juu, yaani wenye uwezo na  siyo walalahoi na kwa tathmini ya haraka utabaini kuwa kundi hilo liko mbali na wale vijana maskini wanaotembea kutwa wakiuza marashi yaliyochanganywa na maji ambayo bei yake hushuka kutoka shilingi 10,000 hadi 5,000.
Kundi hilo la matapeli lina watu nadhifu wanaovaa nguo za bei kubwa. Wanaume wanaokata nywele zao vizuri saluni, wanavaa viatu safi, suti au shati na tai huku mkononi wakiwa na simu za ‘kusugua’.
Kwa upande wa wanawake matapeli wa kundi hilo nao wanavaa vizuri na kuonekana warembo mithili ya washiriki wa mashindano ya kumtafuta Malkia wa Tanzania katika urembo kwenye shindano la Miss Tanzania.
Baada ya kusalimiana wanakuambia kuwa wana biashara ya marashi au pafyumu nzuri kutoka Ulaya au Marekani.
“Dada (au kaka, itategemea wamekutana na nani), nina marashi ya kila aina,” atasema.
“Ni marashi kweli au?”, mteja atauliza.
“Hii pafyumu ni kutoka Ufaransa, Ulaya.”
“Kweli?”
“Kweli, hii pafyumu ni orijino na ukinunua hutajutia uamuzi wako.”
Baada ya utangulizi huo, matapeli hao hufungua mkoba wenye marashi ya aina mbalimbali ambayo hayajachakachuliwa ambayo bei yake halisi ni kati ya Sh 30,000 hadi 200,000.
Matapeli hao wana ujuzi wa kumvuta mteja kwa kuonesha uchangamfu wakati wote wa mahojiano.
“Hii ndiyo saizi yako dada, ukipulizia kwenye nguo huchukua zaidi ya wiki moja,” atakuambia.
“Acha uongo, wiki nzima pafyumu ikae kwenye nguo?”
“Usifikiri ni utani. Hizi ni pafyumu original from France (ni pafyumu halisi kutoka Ufaransa)” ataendelea kutamba mbele yako.
“Bei yake ni shilingi ngapi?”
Akiulizwa swali hilo atakuangalia na kukutathmini, akijiridhisha kuwa unazo, hasiti atakuambia.
“Kila chupa humu kwenye mkoba ina bei yake, kutegemea imetoka wapi na tulinunuaje,” atajibu.
“Bei zinaanzaje?”
“Inategemea kama nilivyosema. Zipo pafyumu za shilingi laki moja, elfu hamsini, elfu thelathini na hata laki na nusu, itategemea… you can buy (unaweza kununua)”
Hutumia lugha nzuri ya biashara na wana uwezo wa kuzungumza sentensi mbili-tatu kwa lugha ya Kiingereza huku wakijigamba kuwa hufuata bidhaa hizo nchi za nje.
Wanaelezea jinsi marashi hayo yanavyonukia vizuri kisha kutoa karatasi laini au kitambaa na kushawishi watu wanuse ili kujua harufu ya manukato wanayotaka kununua.
Hufanya hivyo kwa madai kuwa ni vigumu kusikia harufu ya kutoka katika chupa iliyofungwa vizuri.
Vitambaa hivyo vinanyunyuziwa marashi pamoja na kitu kinachodaiwa kuwa ni sumu au dawa za kulevya.
“Kitambaa hiki kina harufu ya pafyumu hii.”
“Ahaaa kumbe,” atajibu mteja.
“Lakini ukitaka pafyumu hii, nimeipulizia katika kitambaa hiki,” atasema tapeli huku akitoa kitambaa kingine.
Mteja wake akishanusa wanaendelea kuzungumza naye na baada ya dakika chache anasinzia au kulalamika kuwa anajisikia vibaya.
“Najisikia kizunguzungu,” atasema mteja.
“Hee, kwani unaumwa?”
“Hapana, kimenijia ghafla.”
“Hukuwa unaumwa kabla? Pole sana.”
Mteja kizunguzungu kitazidi.
“Usije ukaanguka, hebu keti chini,” atakuambia.
Baada ya dakika chache mtapeliwa atapoteza fahamu akiwa chini na hao matapeli kuanza kazi yao kwa kukulaza chini. Hapo ndipo kundi hilo la matapeli linapopata nafasi ya kuiba na kutokomea kusikojulikana ambako watakwenda kuendelea na wizi mtaa mwingine.
Mtu huyo aliyeibiwa atazungukwa na wasamaria wema na watamkimbiza hospitali na baada ya kufika huko mambo yanakuwa hivi.
“Huyu mgonjwa tumemkuta amelala chini, tunahisi kaleweshwa.”
“Kaleweshwa na nani?”
“Haijulikani kwa sababu tumemkuta akiwa hajitambui.”
Madaktari watampima na kumtundikia drip ya maji ili kuondoa sumu huku wakimpa huduma ya kumpima ili kujua tatizo.
Baada ya kupata fahamu mgonjwa huyo akaeleza kilichomsibu. Alisema watu waliomfanyia unyama huo walitumia mbinu ya hali ya juu ya kujifanya wanauza mafuta mazuri yaani pafyumu.
Alisema walikuwa wamevalia nadhifu kiasi kwamba kwa mtu yeyote haingekuwa rahisi kuhisi kwamba wale wangeweza kuwa matapeli.
“Wanakujia wakiwa hawana wasiwasi na wanakuingia kwa ’gia’ hiyo ya kuuza pafyumu na watakupa maneno matamu ya uongo. Usikubali kuwasikiliza. “Tumeibiwa kwa njia hii watu wengi, kwa mfano yupo mtu mmoja ambaye namfahamu alisema alijikuta akiwa tayari ameibiwa fedha zake zaidi ya shilingi milioni moja baada ya kunusishwa kitambaa kama nilivyofanyiwa mimi,” alisema kijana huyo.
Ni vyema kuchukua tahadhari na kujiepusha kunusa manukato yanayouzwa kiholela na wapita njia hata kama wanatumia magari na kuonekana nadhifu.
Ikiwa mume au mpenzi wako anapenda manukato ni vyema ukamjulisha mbinu hii ya kisasa ya wizi ili ajihadhari na wezi hao.

Post a Comment

Previous Post Next Post