Mawaziri, ma-DC, viongozi wa Serikali matumbo joto

Dar es Salaam. Hatima ya mawaziri na watendaji waliotajwa katika sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow itajulikana Jumatatu ijayo wakati Rais Jakaya Kikwete atakapohutubia taifa kupitia mazungumzo na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Hotuba hiyo ya Rais Kikwete inafanyika ikiwa imepita wiki moja iliyopangwa kukamilisha uchambuzi na kutoa uamuzi dhidi ya wahusika.
Hatua hiyo ya kusogeza mbele muda wa Rais Kikwete kuzungumzia suala hilo inazidi kuwaweka tumbo joto mawaziri na viongozi wengine wanaotuhumiwa kuhusika katika sakata hilo.
Taarifa za awali zilizotolewa na vyombo kadhaa vya habari zilieleza kuwa Rais Kikwete angezungumza jana alasiri, lakini Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilikanusha na kutoa taarifa nyingine, ikieleza kuwa atazungumza Jumatatu.
“Rais Kikwete atazungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa, yakiwamo yale ambayo yamekuwa yanasubiri uamuzi wake tangu alipokuwa anajiuguza kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, baadaye Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa tayari Rais Kikwete ameshatoa uamuzi wake kuhusu suala la escrow na kwamba atautangaza Jumatatu.
Baadhi ya mambo yaliyotokea nchini wakati Rais Kikwete akiwa Marekani alikokwenda kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa tezi dume, ni pamoja na sakata la escrow ambapo Bunge lilipitisha maazimio manane, likiwamo la kumtaka Rais Kikwete kuwachukulia hatua mawaziri na watendaji wa Serikali waliotajwa kuhusika katika wizi wa mabilioni hayo.
Rais Kikwete atatoa hotuba hiyo zikiwa zimepita siku nne tangu alipokatisha ziara ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika Falme za Kiarabu kwa kile alichokieleza kwamba ni kuitwa nyumbani kwa shughuli maalumu, kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu sakata la escrow.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata ndani ya Serikali zinasema kuwa utendaji wa kazi wa baadhi ya mawaziri, wakuu wa wilaya na hata baadhi ya watendaji walioko chini yao umeshuka kutokana na kila mmoja kutojua jinsi uamuzi wa Rais Kikwete utakavyokuwa.
Desemba 9 mwaka huu, Ikulu ilitoa taarifa ya kuwa Rais Kikwete ameshaanza kusoma Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma (PAC) na maazimio ya Bunge kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow na atatoa uamuzi ndani ya wiki moja ijayo.
Katika taarifa hiyo, Rais Kikwete alielekeza kuwa Ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwenye vyombo vya habari vinavyofikia watu wengi kwa ajili ya umma kuisoma na kujua nini hasa kimesemwa na kupendekezwa, jambo ambalo hadi sasa halijafanyika.
Juzi, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema, “Rais Kikwete bado ana nia ya kuzungumza na atafanya hivyo wiki hii kabla ya Jumamosi (leo). Hakusema siku atakayozungumza, alisema atazungumza wiki hii.”
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post