MWAKA WA UCHAGUZI UNAINGIA, WANUNUA UONGOZI WAKAMATWE!


Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Hakuhitajiki kusaka mnajimu au nabii ili kugundua kwamba mwaka 2015 unaoanza Alhamisi ijayo utakuwa na mivutano na misuguano mingi ya kisiasa hapa nchini.
Hili ni jambo linaloeleweka hata kwa mtu ambaye ni mbumbumbu katika masuala ya kisiasa. Mwaka ujao zitafanyika chaguzi za ngazi mbalimbali ndani ya vyama vya siasa kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais kabla ya uchaguzi mkuu.
Chaguzi zote hizi zinalenga kuvipa uhai mpya vyama kwa kupata uongozi kitaifa.
Chama chochote, hata chama cha wacheza ngoma za utamaduni, hakina budi kufanya kazi ya kujikagua kila mara, kwa vipindi vilivyokubaliwa ndani ya chama husika.

Lakini hali tunayoishuhudia ndani ya chama tawala si ya kawaida hata kidogo. Vurugu zilizomo ndani ya chama hicho za watu kujenga makundi ya kuwania uongozi hasa urais zinatisha.
Ni wazi kwamba matatizo ya chama hiki yameanza zamani. Kitakachofanyika ndani ya chama tawala ni kwa kila kikundi ndani yake kuweka utaratibu utakaokiwezesha kikundi hicho kukusanya kura nyingi ndani ya chama tawala kukiwezesha kukamata dola baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Ndiyo maana katika vikumbo tutakavyoshuhudia sasa hatujasikia hata kidogo mabishano ya kifalsafa wala ya kiitikadi, hata ya kisera; tutakachosikia ni minada ya majina ya watu na majina ya vikundi.
Hali hii inanifanya niwe na hofu kuhusu chama tawala na jinsi kinavyojipeleka kuelekea kwenye vurugu kutokana na kulea makundi.

Kwa chama kinachojinasibu kuwa bingwa wa kujenga nchi ya amani na utulivu nchini, kisingekubali kupalilia chuki, ugomvi, fitna, hiyana na kila aina ya uovu miongoni mwa wanachama wake tena vigogo.
Ukweli ni kwamba uhasama uliomo ndani ya chama tawala haupo kati ya chama hicho na vyama vya upinzani bali vigogo wenyewe kwa wenyewe.

Naweza kusema kuna mgando wa hisia kwani kuna wanasiasa wanaona ni lazima rais awe anatoka katika kundi lao.  Mgando huo wa hisia hauruhusu kufikiri kwamba inawezekana safari hii rais asitoke katika kundi lao hata kidogo. Hisia zilizoganda haziruhusu kutambua kwamba nchi imebadilika kiasi kwamba waliokuwepo mwaka 1961 kuendeleza chama ni wachache ikilinganishwa na wale waliokuja baada ya Uhuru.
Kuna vitu vingi vinakila chama tawala hasa mambo ya ufisadi kama haya ya akaunti ya escrow, kugawiana nyumba za serikali, kupora fedha Benki Kuu na kujizawadia migodi ya taifa.Lakini mgando wa ubongo unawatia hamasa wana makundi ndani ya chama-tawala kuchambana, kushutumiana, kutukanana, kuwindana, kuhujumiana, na wataendeleza zaidi   kasi ya mapambano yao mwaka 2015.
Wengi tunajua vigogo wachache wanavyotumia fedha kununua nafasi za utawala. Viwango vya fedha vinavyoendelea kutumika katika chaguzi zetu tunavijua? Ni nyingi, zinatoka wapi?
Fedha hizo zinatoka wapi? Vyanzo vyake ni vipi? Hivyo vyanzo vina maslahi gani katika nchi hii?
Tujiandae kuona katika mwaka ujao wakubwa wa vyama vya siasa wakipigana vikumbo kukusanya fedha haramu kwa ajili ya kununua nafasi za uongozi. 

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema, yeye alikaa ikulu zaidi ya miaka 24, hakuna biashara pale, hawa wanaokusanya mamilioni ya fedha za kampeni watazirudishaje?
Sheria zipo zilizotungwa ili kuzuia fedha haramu zisiingizwe katika uchaguzi, lakini sheria hizo hazifanyi kazi! Asasi za kuzuia rushwa zimeundwa, na hata kupewa majina kama PCCB, lakini ni kama mdoli, hawawakamati wanaonunua uongozi.
Yote hii ni kwa sababu watungaji wa sheria hizo na wasimamizi wa utekelezaji wake, hawakuwa na nia na wala hawana nia, ya kuziruhusu zifanye kazi kwa sababu wao ndiyo wahalifu wakubwa dhidi ya sheria hizo.
Natoa changamoto kwa yeyote katika asasi za kupambana na kuzuia rushwa, udhibiti wa mienendo ya vyama vya siasa, sekretareti za maadili na asasi nyingine zinazoendeshwa kwa gharama kubwa za kodi za wananchi wa Tanzania, wasimame kuhakikisha kuwa mwakani rushwa ya kununua uongozi inadhibitiwa.
Asasi kama hizi zilianzishwa katika nchi nyingi zilizoendelea ili angalau kupunguza vitendo vya ufisadi katika michakato inayotakiwa kuwa mitakatifu, kama vile uchaguzi.Katika nchi hizo, kwa kiwango kikubwa asasi hizi na sheria zake zinafanya kazi, na mara kwa mara wahalifu hukamatwa na kuadhibiwa, kwa nini hapa tusishuhudie hayo na wanaovunja sheria wapo?
Haya ni masuala ya kutafakari wakati tukiuanza mwaka ujao ambao bila shaka utakuwa na mikwaruzano mingi ndani ya vyama, mabishano yenye hamasa kuhusu mustakabali wa taifa letu, hasa kuhusu kura ya maoni ya Katiba Mpya.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Post a Comment

Previous Post Next Post