Mwenyekiti wa kijiji, mkewe wachinjwa

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangahe, kilichopo Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, aliyechaguliwa hivi karibuni, Mussa Chotta na mkewe, Mariamu Mhoja, wameuawa kikatili kwa kukatwakatwa na mapanga.
Chotta, ambaye alichaguliwa na wananchi kushika wadhifa huo katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Desemba 14, mwaka huu, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliuawa na watu wasiofahamika usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake katika Kitongoji cha Bukili.

Kaimu Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Bagaile Lumolla, alithibitisha kuuawa kwa Chotta na mkewe.

Alisema tukio hilo lilitokea nyumbani kwa marehemu katika kitongoji hicho kilichopo katika kijiji cha Nyangahe kata ya Bukumbi wilayani humu.

Hata hivyo, Lumolla alisema chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana huku baadhi ya wananchi waliohojiwa na NIPASHE wakilihusisha na itikadi za kisiasa. 

Mtoto wa marehemu, Masumbuko Chotta, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa watu hao ambao walikuwa watatu baada ya kufanya mauaji hayo, walitoweka.

Akisimulia zaidi tukio hilo, Masumbuko alisema yeye na wadogo zake wakati wakiwa wamelala chumbani kwao, ghafla walisikia kishindo kikubwa kikipigwa mlangni.

Alisema waligundua baadaye kuwa waliohusika na kishindo hicho ni maharamia waliokwenda kutoa roho za baba na mama yao.

“Mara baada ya mlango kufunguka, watu hao waliingia ndani na kwenda moja kwa moja chumbani kwa baba na mama na kuanza kuwashambulia kwa kuwakata na mapanga ovyo ovyo mwilini na kusababisha vifo vyao,” alisema Masumbuko.

Alisema walijaribu kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani, lakini mmoja wa watu hao alimpiga kofi na kuanguka chini kisha kupoteza fahamu.

Jeshi la Polisi wilayani humu limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Juma Bwire, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.

Msaidizi wa Kamanda Bwire alisema bosi wake yupo kwenye kikao na kumshauri mwandishi wa habari hii amtafute baadaye.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post