Katuni
Taarifa hiyo pia ilisema kuwa Rais Jakaya Kikwete, alikubali ombi la kujiuzulu kwa Jaji Werema na kwamba amemshukuru kwa utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu.
Jaji Werema anatajwa kuwa kitovu cha watumishi wote wa umma wanaotajwa kuhusika na sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, akiwa ametoa ushauri kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, juu ya utoaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti hiyo ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Anatuhumiwa kwamba ushauri wake ulifanikisha kuchotwa kwa fedha hizo ambazo zimeibua mgogoro mkubwa wa uadilifu kiasi cha kuifikisha serikali kwenye mtego mbaya wa kuanguka baada ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilishwa bungeni wakati wa mikutano ya Bunge ya 16 na 17.
Kujiuzulu kwa Jaji Werema ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya watu wote waliohusika na kashfa ya uchotwaji wa fedha za Escrow kuwajibishwa na mamlaka za uteuzi. Katika orodha ya vigogo wanaotakiwa kuwajibika pia wamo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa anna Tibaijuka na Maswi. Wote wanatakiwa mamlaka za uteuzi wao ziwavue nyadhifa zao.
Tangu kuanza kuchemka kwa sakata hili katikati ya mwaka huu, serikali kwa ujumla wake au kupitia kwa kiongozi mmoja mmoja, imekuwa na tabia ya kutaka kufunika jambo hili kwa utetezi kwamba eti fedha zilizokuwa kwenye Tegeta Escrow siyo za umma, ama sehemu yake au hata zote kwa ujumla.
Waliosimama na kutetea kwamba fedha hizo hazilikuwa ni za umma ni pamoja na Werema mwenyewe, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Profesa Muhongo na hata Maswi katika nyakati na maeneo tofauti. Wapo waliozungumzia bungeni lakini wengine kwenye majukwaa tofauti.
Katika kundi la viongozi wenye nyadhifa za uteuzi wa rais, Profesa Tibaijuka anatakiwa kuwajibishwa kwa kuwa alipokea mgawo wa zaidi Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa aliyekuwa mwanahisa wa IPTL, James Rwegamalira anayedaiwa kugawa fedha kama njugu kwa watu wengi, wakiwamo mawaziri wa sasa na wa zamani, watendaji serikalini, viongozi wa dini, waandishi wa habari na wanasiasa kadhaa.
Kuachia ngazi kwa Jaji Werema katika kipindi kama hiki siku 18 tangu Bunge litoe maazimio manane juu ya wahusika wote wa kashfa ya Tegeta Escrow, siyo tu ni uamuzi uliochelewa bali ni dalili kwamba uamuzi wake umefikiwa kutokana na shinikizo. Kimsingi haoni kuwa amefanya makosa. Uamuzi wa kujiuzulu hakupaswa kusubiri muda wote huo.
Hata hivyo, kuondoka kwa Jaji Werema kunaweka mambo katika mstari mmoja kwamba sasa maazimio ya Bunge yanaanza kutekelezwa. Ni habari njema kwamba pamoja na kuchelewa kuchukuliwa kwa hatua sawasawa na maazimio hayo sasa uwajibikaji umeanza kuonekana.
Ni matumaini yetu ya juu kabisa kwamba wengine waliosalia katika orodha ya wote wanaotakiwa kuwajibika au kuwajibishwa watafuata mkondo wa Jaji Werema. Kwa kufanya hivyo watakuwa wanasaidia taifa hili kupiga hatua nzuri za maendeleo katika nyanja za uwajibikaji na utawala bora.
Hata hivyo, tunatoa hadhari kwamba isije ikawa kwamba kujiuzulu kwa Jaji Werema ndiyo mwanzo na mwisho wa uwajibikaji katika kashfa ya Escrow.
Tunasema hivyo kwa sababu kwa kitambo sasa kumekuwa na juhudi ambazo zina sura ya mkono wa dola kutaka kupindisha ukweli juu ya maazimio ya Bunge na uhusika wa baadhi ya viongozi hasa wa Wizara ya Nishati na Madini. Kuna juhudi za kutaka kuwaepusha na mkondo wa uwajibikaji.
Kuna kampeni kubwa inayoendeshwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari ikieleza kuwa wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini wamefanya kazi kubwa tangu wapewe dhama hiyo, wamesifiwa kama wakombozi wa sekta ya nishati na madini nchini.
Siyo madhumini ya tahariri hii kuingia kwenye undani wa ukweli au upotoshwaji wa sifa zinazomiminwa kwa wakuu hao, ila itoshe kusema tu mbele ya umma suala linalosubiri uwajibikaji ni la uchotwaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow. Hakuna jambo jingine hapa. Hakuna anayetazama jambo nje ya hilo. Ni akaunti ya Tegeta Escrow basi.
Tunaamini serikali na wote wanaotaka kujenga taswira kinyme na kilichotokea bungeni mwezi uliopita wajue kwamba kutokutekelezwa kwa maazimio ya Bunge ni kukaribisha balaa katika taifa hili. Balaa hili litaendelea kuitikisa serikali na taifa kwa ujumla.
Kashfa ya Tegeta Escrow ni moja ya kielelezo cha kupima uwajibikaji na utawala bora kwa wote wanaoguswa na sakata hilo. Tunawaambia wote waliotakiwa kujizulu au kuwajibishwa wafuate mkondo wa Jaji Werema ili taifa sasa litulie na kutazama mambo mengine ya muhimu kwa ustawi wake kabla mwaka haujamalizika.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment