Sukari ya magendo yatamba Dar

  Kilo yauzwa kwa Sh.1000, Mafuta pia yashika usukani.
Wakati maelfu ya tani za sukari yakidaiwa kurundikana kwenye maghala ya viwanda vya sukari nchini, bidhaa mbalimbali ikiwamo sukari ya magendo inayouzwa kwa bei ya chini imeendelea kuingia nchini kupitia bandari bubu mbalimbali zikiwamo za jiji la Dar es Salaam, NIPASHE imethibitisha.
 Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa takriban wiki tatu katika maeneo ya fukwe za Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, hasa eneo la Mbweni wilayani Kinondoni, umebaini kuwa wafanyabiashara wamekuwa wakiingiza sukari kutoka nje ya nchi ikiwamo ya India ambayo huuzwa kwa kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 60,000 kwa mfuko wa kilo 50 ambayo ni sawa na Sh. 1,000 hadi Sh. 1,200 kwa kilo moja.

 Uchunguzi umebaini vilevile kwamba bei ya sukari hiyo hupanda au kushuka kulingana na hali ya upatikanaji wake na mnunuzi wa jumla hupata nafuu zaidi kwa kuwa usafiri hutolewa na wauzaji hao wa njia za magendo.

 Bei ya sukari kutoka nje ni ya chini kulinganisha na ile inayozalishwa kwenye viwanda mbalimbali vya sukari nchini. Katika maduka ya jumla eneo la Manzese jijini Dar es Salaam, bidhaa hiyo iliyozalishwa kwenye Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, yenye uzito wa kilo 20, huuzwa kwa Sh. 32,500, sawa na Sh. 1,625 kwa kilo moja, wakati sukari ya nje yenye uzito wa kilo 50 huuzwa kwa Sh. 70,000 hadi Sh. 73,000 sawa na Sh. 1,400 hadi 1,460 kwa kilo moja.

 Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo la Mbweni, ambaye jina linahifadhiwa, alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa mnunuzi anayechukua sukari ya ujazo mkubwa wa walau kuanzia mifuko 20 ya kilo 50, husafirishiwa mzigo hadi dukani kwake au kwenye eneo lolote atakalo jijini Dar es Salaam ili kumwepusha na usumbufu wa polisi.

“Kama utachukua mzigo mkubwa usafiri utakuwa juu yangu… utaletewa hadi mlangoni ili polisi wasikusumbue njiani,” alisema mfanyabiashara huyo.

Alimfafanulia mwandishi wa habari hii kwamba biashara hiyo ina changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kufuata mzigo wakati wowote unapokuwa tayari, hata kama ni usiku.

 “Leo mzigo utaingia saa tisa usiku... ni uhakika kabisa. Unaweza kuja kuona, pengine utapenda biashara nyingine zaidi maana inakuja mizigo mingi,” alisema.

Mwandishi wa habari hizi alipotaka kujua aina nyingine ya bidhaa anazoweza kupata, alitajiwa kuwa ni pamoja na betri za magari na mafuta ya kula.

 DUKANI KWA MFANYABIASHARA
 Ukifika dukani kwa mfanyabiashara huyo, kamwe huwezi kubaini kama ni mtu anayefanya biashara kubwa ya jumla.

Duka hilo linauza bidhaa ndogo ndogo za matumizi ya kila siku nyumbani ikiwamo sukari ya kupima ya Kilombero, mafuta ya kula ya kupima, dawa za kuulia wadudu, sabuni za kufulia za unga na za mche, dawa za meno, mafuta ya kupaka, unga wa sembe na mahitaji mengine kadhaa.

 Aidha, wafanyabishara wa eneo hilo jumla hufanya kazi kwa tahadhari kubwa ikiwa ni pamoja na kutofanya biashara na mtu wasiyemjua na hivyo huwa si rahisi kwa mnunuzi kwenda moja kwa moja kuuliza sukari au mafuta ya jumla bila kupelekwa na mkazi wa eneo hilo au mfanyabiashara mwenzake ambaye amewahi kufanya kazi naye.

 WANANCHI MBWENI
 Hatua ya kwanza ya mwandishi ilianzia kwenye ufukwe wa bahari ambako alikutana na wafanyabishara wa samaki katika bandari ‘bubu’ ya Mbweni.

 Msamaria mwema alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba eneo hilo lina biashara nyingi ambapo mbali na samaki wanaopatikana zaidi siku za Ijumaa, pia kuna biashara za mafuta na sukari ambazo mara nyingi hufanyika nyakati za usiku.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alihudhuria mnada wa samaki kwenye eno hilo, aliulizia zaidi kuhusu biashara ya sukari na mafuta kwa kijana mwenye kibanda kimojawapo cha kuuzia vinywaji baridi kama maji na soda katika eneo hilo baada ya kutambulishwa na mmoja wa kina mama wauzao samaki.

 “Achana kabisa na biashara hii, kama umeamua kuuza samaki endelea nayo tu maana huku (kwenye sukari), kuna mambo mengi,” alisema.

Hata hivyo, kabla hajatoa ufafanuzi huo, kijana huyo aling’aka na kuhoji: “Kwani umekuja kuangalia samaki au sukari?”

 Msamaria mwema ambaye alimtambulisha mwandishi alidakia na kusema: "Maisha ni kuhangaika huku na huku, ndiyo maana tunauliza... msaidie huyu ndugu yangu."

 Baada ya maelezo hayo, kijana huyo alishauri kwamba ni vyema mfanyabishara mwenye mtaji mdogo wa samaki asiingie kwenye biashara ya sukari katika eneo hilo.

Baada ya kuachana na kijana huyo, mwandishi wa habari hizi ambaye tayari alishakuwa na marafiki kadhaa kutoka miongoni mwa kina mama wanaonunua samaki eneo hilo, aliondoka na wakati wakiwa njiani, alielezwa kuwa kijana mwenye banda anafanya biashara ya sukari kwa kushirikiana na wenye maduka ya jumla eneo la Mbweni Mwisho.

 DUKANI MBWENI MWISHO
 Msamaria mmoja mwenye duka eneo la Mbweni mwisho aliiambia NIPASHE kwamba biashara ya magendo ni kubwa eneo hilo na kwamba wafanyabiashara wanaingiza zaidi sukari na mafuta.

Msamaria huyo alimpeleka mwandishi kwa mfanyabiashara wa sukari na kwa kijana mwingine anayejihusisha na biashara hiyo, hivyo NIPASHE ilifanikiwa kununua mfuko mmoja wa kilo 50 kwa Sh. 60,000 ambayo imetolewa kwa watoto yatima.

 Sukari katika maduka mawili yanayofanya biashara ya magendo katika eneo hilo ambayo NIPASHE ilifika, inaingia usiku au mapema alfajiri.

NIPASHE ilishuhudia shehena ya sukari kwenye maduka hayo ingawa ilinunua mfuko mmoja kwa Sh. 60,000, haikupungua sana bei kwani nafuu ni kwa wanaonunua mifuko mingi kwa mpigo. Anayenunua zaidi ya mfuko mmoja ndiye huuziwa kwa Sh. 50,000.

Sukari hiyo ya NIPASHE ambayo imepelekwa kwa watoto yatima, ilisafirishwa kwa usafiri wa kawaida kutoka Mbweni hadi Tegeta na kisha hadi Mwenge bila usumbufu wowote kutoka kwa maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

WASAMBAZAJI WA JUMLA
 Baadhi ya wauzaji wa jumla wa sukari ambao wamepewa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi, waliiambia NIPASHE kwamba bei ya sukari inayozalishwa nchini ni kubwa na ndiyo inayoyumbisha biashara hiyo.

Wauzaji hao ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini, walisema sukari ikishakuwa na tofauti ya Sh. 50, huwa ni kikwazo kwa wafanyabishara wa jumla na rejareja.

 “Tatizo ni bei kubwa ya sukari ya viwanda vyetu na mbaya zaidi, ukitaka kununua sukari nyingi kwenye viwanda vyetu hupati... lakini tunashangaa kusikia wanalalamikia soko,” alisema mmoja wa wauzaji wa jumla.

 MADUKA YA JUMLA MANZESE
 Katika maduka mengi ya jumla eneo la Manzese, sukari ya Kilombero yenye uzito wa kilo 20 huuzwa kwa Sh. 32,500 ambayo ni sawa na Sh. 1,625 kwa kilo moja.

Katika eneo hilo, sukari ya nje yenye uzito wa kilo 50 huuzwa kwa Sh. 70,000 hadi Sh. 73,000 ambayo ni sawa na Sh. 1,400 hadi 1,460 kwa kilo moja.
 Sukari katika maduka mengi ya rejareja jijini Dar es Salaam huuzwa kwa Sh. 1,800 hadi Sh. 2,000 kwa kilo moja.

 WENYE VIWANDA
 Takwimu za mwezi uliopita zilizotolewa na kiwanda cha sukari Kilombero zilieleza kuwa tani 158 za sukari zimeharibikia kwenye ghala la kiwanda hicho mkoani Morogoro mwaka jana huku tani 40,000 zikishindwa kuuzika kutokana na kuendelea kuingizwa kwa sukari kutoka nje ya nchi inayouzwa kwa bei ya chini inayoathiri mauzo ya sukari wanayoizalisha wao.

Mwenyekiti wa wamiliki wa viwanda vya sukari nchini, Mark Bainbridge, alikaririwa akisema kuwa kutokana na hali hiyo, wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za uendeshwaji wa kiwanda ikiwamo kuwalipa wafanyakazi mishahara na kwamba, kama hali itaendelea kuwa hivyo, watavifunga viwanda na kutafuta kazi nyingine za kufanya.

 Alisema kwa miaka minne mfulululizo, wamekuwa wakisumbuliwa na hali hiyo ya uingizwaji wa sukari ambayo haitozwi kodi na matokeo yake, inapoingia huuzwa kwa bei sawa na wao au chini kidogo na hivyo kuwapunguzia uwezo wa kushindana nayo sokoni.

Hata hivyo, aliitaka jamii na pia serikali kutambua ukweli kuwa siyo kwamba wao hawataki sukari kutoka nje iingie nchini, bali iingizwe kwa taratibu zinazoeleweka, hususan panapokuwa na mahitaji na siyo sasa hivi ambako sukari imekuwa nyingi katika viwanda vya nyumbani, lakini bado inaingizwa nyingine kwa wingi zaidi kutoka nje.

Akizungumza na NIPASHE mwishoni mwa wiki, Meneja Kilimo wa kiwanda cha Sukari Kilombero-Ilovo, Joseph Rugaimukamu, alisema hadi mwishoni mwa Novemba, 2014, kiwanda chao kilikuwa na tani za sukari 40,000 ambazo hazijauzika mpaka sasa.

 “Hapa tunafanya tu juhudi za ndani ili tuendelee kuishi, ili tunusuru maisha ya wafanyakazi wetu,” alisema.

 Alisema tatizo linalovikabili viwanda vya sukari kama chao cha Kilombero lina athari kubwa kwenye uchumi wa nchi kwa kuwa linawaumiza wafanyakazi, wakulima na serikali kwa ujumla kwani baadhi ya wafanyabishara wanaoingiza sukari kutoka nje huwa hawalipi kodi na hivyo kutumia njia za magendo.  Alisema pamoja na kwamba sukari inayotoka nje inauzwa kwa bei chee kwa wafanyabiashara wa jumla, lakini haimnufaishi Mtanzania wa kawaida kwa kuwa bei ya rejareja ni Sh. 1,800 hadi Sh. 2,000.

 Kwa mujibu wa Bainbridge, uhitaji wa sukari kwa mwaka hapa nchini ni tani 420,000, lakini uwezo wa uzalishaji wa viwanda ni tani 320,000; hivyo uhaba wa tani 100,000 hutokea pale viwanda vinaposimamisha uzalishaji, ambako mara nyingi huwa ni katika kipindi cha msimu wa mvua za masika.

 WAKULIMA
 Kwa upande wao, baadhi ya wakulima wa miwa walisema hali ni mbaya na kuitaka Serikali hususan Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuingilia kati suala hilo kwa kuwa aliwaahidi kufanya hivyo wakati walipomfuata bungeni kwa ajili ya kupeleka kilio chao.

Kutokana na mgogoro huo, bei ya miwa imeshuka kutoka Sh. 69,000 kwa tani hadi kufika Sh. 55,000 kwa tani.

 MAFUTA YA KULA
 Hali ya mafuta ya kula haitofautiani na sukari kwa kuwa mafuta ya aina mbalimbali huingia nchini kinyemela na kuuzwa kwa bei ya kutupa.

Katika eneo la Mbweni, mfanyabishara ambaye ni kitovu cha biashara hizo za magendo huuza mafuta aina ya Premier, Viking, Oki na Turky yenye ujazo wa lita 20 kwa Sh. 37,000 hadi Sh. 40,000 wakati kwenye maduka ya jumla eneo la Manzese, mafuta hayo yanauzwa kwa Sh. 40,000.

 Manzese mafuta ya kula bei ya jumla yanayozalishwa nchini yenye ujazo wa lita 20 yanauzwa kwa Sh. 56,000 hadi Sh. 58,000 wakati yaliyo kwenye ujazo wa lita 10 aina ya Sundrop na Korie yanauzwa kwa Sh. 24,000.

 Uchunguzi umebaini kuwa mafuta yanayozalishwa nchini kwa bei ya jumla yanauzwa Sh. 2,400 hadi 2,900 kwa lita moja wakati mafuta yanayotoka nje yanauzwa kwa Sh. 1,850 hadi Sh. 2,000 kwa lita; hali ambayo inawafanya wananchi kununua zaidi mafuta ya nje kwa kuwa ni nafuu.

 JESHI LA POLISI
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, aliiambia NIPASHE kwamba TRA, ndiyo yenye wajibu wa kuzuia biashara ya magendo kwa kuwa wanaofanya biashara hiyo hukwepa kodi.  “Naomba uongee na mamlaka ya mapato (TRA)... kazi yao ni kukusanya mapato na pia kupambana na kuzuia wakwepa kodi. Hili ni jukumu lao na wanapaswa kuliongelea. Niulize kuhusu uhalifu mwingine wa jinai ambao hakuna wa kuongelea isipokuwa polisi,” alisema Wambura katika ujumbe wake wa simu aliotuma kwa NIPASHE.

 TBS WACHUNGUZA
 Kwa upande wake, Shirika la Viwango (TBS), limesema tayari wamechukua sampuli za aina kadhaa za mafuta ambazo wanazifanyia uchunguzi ili kujua ubora wake.   Mwanasheria wa TBS, Baptister Bitaiso, aliiambia NIPASHE kwamba kazi hiyo inafanyika na wakati wowote majibu yatatolewa na kuahidi kufanya uchunguzi kwenye sukari pia.

 NCHEMBA ATANGAZA MSAKO
Mapema mwezi uliopita, Serikali ilitangaza msako mkali dhidi ya wanaoingiza sukari nchini na wauzaji wa sukari ya magendo na kusababisha athari za kiuchumi.

 Tangazo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Mwigulu Nchemba, wakati wa ziara yake ya siku moja kwenye kiwanda cha kuzalisha Sukari cha Kagera (KSL), baada ya Meneja Mkuu wa KSL, Ashwin Rana, kueleza kuwa sukari inayoingizwa nchini kwa magendo imekuwa tishio kwa ustawi wa kiwanda hicho.

 TRA WAUNDA ‘FAST TEAM’
 Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alipoulizwa mamlaka hiyo inachukua hatua gani kudhibiti biashara hiyo, alisema TRA imeunda kikosi maalum cha kufanya doria kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi.

"Kama unavyojua hizi biashara zinafanyika kwa siri sana, na zinafanywa na watu ambao nao wamejipanga kukabiliana na sisi. Tunafanya kila juhudi kwa kufanya doria kupitia kikosi maalum cha 'fast team' na tunategemea taarifa za wasamaria wema na tumekuwa tukitoa zawadi kwa wale wanaofichua na kufanikisha kukamatwa kwa bidhaa zisizolipiwa kodi," alisema.

 Aliongeza kuwa mikakati mingine ni kutaifisha gari au nyumba itakayokutwa imehifadhi mali za magendo.

"Tukikamata mzigo tunatangaza na sasa hivi tunataifisha gari au nyumba itakayokutwa imehifadhi mali ya magendo, hizi ni hatua ambazo TRA inachukua kukabiliana na tatizo hili."  Hata hivyo, Kayombo alipoulizwa kikosi hicho kimefanikiwa kiasi gani na ni watu wangapi au mali kiasi gani imekamatwa hadi sasa, alisema hana taarifa kamili na kuomba apewe muda zaidi wa kutafuta takwimu.

Alisema bandari bubu kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi kuanzia Dar es Salaam hadi Mombasa ni nyingi na zinahitaji jitihada za wasamaria wema kuisaidia TRA.

 Alitoa mfano kuwa mpaka wa Tanzania na Malawi mkoani Mbeya ni mdogo, lakini una njia 32 za panya; hivyo za Bahari ya Hindi ni nyingi zisizo na hesabu.

 Alisema maeneo kama Ununio, Msasani, Mbweni, Mbegani, Kaole na fukwe za Bagamoyo, kuna njia za panya nyingi zisizo na idadi.

 Hata hivyo, baada ya kutoa majibu hayo kwa NIPASHE, alimwomba mwandishi huyu ampeleke kwa watu wanaoingiza bidhaa hizo akieleza kuwa ni watu hatari ambao pia wanatishia uhai wa maofisa wa TRA.

 Aidha, kabla TRA haijatoa majibu kwa NIPASHE, ilitoa tangazo kwa vyombo vya habari likifafanua kile NIPASHE ilichokuwa imehoji, likiwatahadharisha wafanyabiashara na watu wanaoishi katika ukanda wa Pwani maeneo ya Saadani, Mbweni, Mlingotini, Ununio, Kawe, Msasani, Kunduchi, Kigamboni na Kisiju kujihadhari na biashara ya magendo.

 Taarifa hiyo ilitaja bidhaa zinazohusishwa kwenye biashara hiyo kuwa ni sukari, mafuta ya kupikia, mchele, maziwa ya unga, betri za tochi na nguo; na kufafanua kuwa watakaokamatwa wakifanya biashara ya aina hiyo watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na mali zao kutaifishwa.

 “Uingizaji bidhaa nchini bila kulipa kodi ni ukiukaji wa sheria ya forodha ya mwaka 2004… wananchi wote na hasa wa maeneo yaliyotajwa wanaombwa kutoa taarifa pale wanapoona mali zilizotajwa au nyinginezo zikiteremshwa kwenye bandari bubu,” lilisema tangazo hilo.

 KAMATI YA PAC
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeahidi kuanza kufuatilia sakata la kuingizwa nchini kiholela kwa sukari kutoka nje kufuatia malalamiko ya wamiliki wa viwanda vya sukari yanayotolewa kutokana na soko la ndani kutekwa na sukari inayoingizwa kutoka nje ya nchi na wafanyabiashara wakubwa.

 Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alikaririwa akisema kuwa tayari wameiita Bodi ya Sukari kwa ajili ya kujadiliana nao kwa kina kuhusu suala hilo.

 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post