TAHADHARI: Dawa za ‘kutibu meno bila kung’oa,’ zinaathiri afya

Matatizo katika afya ya kinywa na meno yamekuwa changamoto kwa watu wengi si tu nchini bali sehemu mbalimbali ulimwenguni.
Watu wengi wamekuwa wakilalamika vinywa kutoa harufu mbaya kama uvundo, fizi kutoka damu pamoja na kutoboka kwa meno kunapoambatana na maumivu makali kwa mhusika.
Hali hiyo imekuwa ni changamoto ambayo imesababisha kuibuka kwa waganga mbalimbali wa jadi (asili) wanaojinadi na kujinasibu kwamba wana uwezo wa kutibu matatizo yote yanaambatana na hitilafu katika afya ya kinywa.
Katika maeneo ya mijini ni jambo la kawaida kukutana na waganga wa aina hii wenye kudai kuwa wana uwezo wa kutibu jino bila kung’oa, kuthibiti harufu mbaya ya kinywa na fizi kutoa damu. Si mijini tu hata vijijini waganga hawa wapo.
Wengine wamekuwa wakijitangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kutokana na kukua kwa teknolojia na utandawazi matangazo yao yamewavuta wengi na wengi wametumia dawa hizo na baadhi kusifu kuwa zimewasaidia wamepona. “Nusura ning’oe jino, lakini nilipotumia dawa suala la kung’oa likaisha.” Baadhi husikika wakisifu.
Je kuna ambaye aliwahi kujiuliza kama kweli dawa hizo zinatibu na hazina madhara kwa watumiaji?
Je kuna ambaye aliwahi kufikiri kuwa dawa hizo hazitibu bali husababisha ganzi tu katika mishipa ya fahamu kiasi cha kumfanya mgojwa aamini kuwa amepona jino na halina haja tena kung’olewa?
Je kuna aliyewahi kujiuliza kuwa matumizi ya dawa hizo mbali ya kuleta madhara katika mishipa ya fahamu pia huweza kusababisha saratani ya kinywa?
Dk Jacob Chembele wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma anaeleza kwa kina juu ya afya kinywa na kufafanua matumizi ya dawa holela huweza kusababisha madhara mengine ikiwemo saratani ya kinywa na hata kifo.
Dk Chembele anaanza kwa kufafanua nini maana ya afya ya kinywa na namna sahihi ya utunzaji wa afya ya kinywa inayopendekezwa kitaalamu ikiwemo matibabu pindi inapohitajika.
Anasema afya ya kinywa ni hali ambayo kinywa na meno hufanya majukumu yake kwa ufanisi na tija ya hali ya juu.
Majukumu hayo ni pamoja na mwonekano mzuri wa uso, kutamka herufi au maneno vizuri na kula chakula.

Post a Comment

Previous Post Next Post