Umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi unaonekana kutokana na
ukweli kwamba rasilimali watu ni suala la muhimu katika mchakato wa
maendeleo.
Bila ya rasilimali watu, vigezo vingine kama mtaji, ardhi na rasilimali nyingine haviwezi kuwa na manufaa yoyote.
Hata hivyo, rasilimali watu itakuwa na tija kama
tu itapewa nyenzo na ujuzi ili kuboresha utendaji na ufanisi. Hiki
ndicho hasa elimu na mafunzo ya ufundi inalenga kukifanya.
Tangu baada ya mapinduzi ya viwanda katika nchi za
Ulaya Magharibi katika karne ya 18 na 19, maendeleo na mafanikio ya
elimu ya ufundi, vimenasibishwa kwa karibu na maendeleo ya kiuchumi. Na
maendeleo yoyote ya kiuchumi ya nchi husika hutokana na ubora wa
rasilimali watu wa nchi husika.
Ubora huu wa rasilimali watu hutokana na ubora wa
mfumo wa elimu wa nchi husika. Elimu na mafunzo ya ufundi inachukuliwa
kama ni mojawapo ya vigezo muhimu katika kukuza uzalishaji na uchumi kwa
jumla.
Katika kufanikisha hili, shule na vyuo vina jukumu
la kuandaa na kuzalisha nguvukazi yenye ujuzi wa kutosha ili kuongeza
ufanisi kazini.
Kama anavyosema mwandishi aitwaye Giroux, elimu na
mafunzo ya ufundi nyakati zingine huwa ni zana ya kutatua matatizo ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii ambayo yanatishia uimara wa kiuchumi na
kisiasa wa baadhi ya mataifa.
Kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira na
mabadiliko ya namna ya utendaji kazi, yameliweka suala la elimu ya
nguvukazi kuwa lenye kipaumbele cha juu katika uboreshaji wa mifumo ya
elimu.
Katika utafiti nilioufanya mwaka 2009 wilayani
Temeke, nilibaini kuwa wahojiwa wengi walikiri kuwa elimu na mafunzo ya
ufundi vilikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu; na
vyuo vya ufundi viliandaa wahitimu wa kutosha kutokana na mahitaji ya
nchi kwa wakati huo.
Aidha, walikiri kuwa elimu na mafunzo ya ufundi
ilikuwa bora zaidi ukilinganisha na elimu ya taaluma katika kukuza
ujuzi, teknolojia na ujasiriamali.
Pia, kwenye uwezo wa kujiajiri watahiniwa wa vyuo
vya ufundi walionekana kuwa na uwezo zaidi ukilinganisha na watahiniwa
katika elimu ya kawaida.
Utafiti ulibaini kuwa vyuo vya ufundi vya umma
vinaweza kupata mafanikio zaidi pamoja na ufanisi wa hali ya juu kama
vitaendeshwa kibiashara.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment