Yona: Nilimshauri Mkapa kuleta kampuni ya kukagua dhahabu

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,Daniel Yona.
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (pichani), ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alimshawishi Rais Benjamin Mkapa kukubali mkaguzi wa dhahabu kufanya ukaguzi wa madini hayo kutokana na umuhimu wake wakati ule.
Alisema hayo wakati akijibu utetezi alioutoa Septemba 19, mwaka huu katika kesi  inayomkabili ya matumizi mabaya ya ofisi ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.

Aidha, alisema aliwahi kumuandikia Rais Mkapa kuomba kibali cha kumleta mkaguzi huyo bila kutaja kiasi maalum cha gharama.

Akijibu swali la Wakili wa upande wa Mashtaka, Frederick Kimaro, Yona aliambia mahakama kuwa njia zilizotumika kuipata kampuni hiyo ya ukaguzi zilifuata taratibu, kanuni na sheria zinazohusiana na ugawaji wa tenda kwa kampuni.

Wakili Kimaro alimuuliza Yona ni kwa nini barua aliyoiandika kwa rais haikutaja kiasi cha fedha ambacho alitakiwa alipwe mkaguzi badala yake iliandikwa kwa kukadiria.
Yona alieleza mahakama kuwa hakuweza kuandika maelezo moja kwa moja kwa sababu malipo ya mkataba huo yalikuwa yanaendelea kufanyiwa tathmini na wataalam wake kuhusu gharama za kuilipa kampuni hiyo ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.

Wakili Kimaro alimuuliza Yona kwamba kabla ya kumuandikia rais madokezo ya barua kuhusu zabuni hiyo, alikuwa amepata ushauri kutoka sehemu yoyote na ulichukulia uzito gani ushauri huo?

 Yona alijibu kuwa alipokea taarifa za ushauri kutoka sehemu mbalimbali ikiwamo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini akitakiwa kufanya uchunguzi kabla ya kutoa zabuni kwa kampuni hiyo.

Aldai kuwa aliiachia kamati yake kulishughulikia suala hilo.

Mbali na Yona, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na Katibu Mkuu wa zamani wa  Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.

Baada ya mahojiano hayo kati ya Yona na Wakili Kimaro kumalizika, Jaji John Utamwa aliihairisha kesi hiyo hadi Machi 16-20, mwakani.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post