Musoma. Mwanamke mmoja mkazi wa Kata ya Buhare,
Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Helena Paulo (20), amejifungua watoto
pacha wa kike walioungana eneo la kifuani hadi tumboni wakiwa na uzito
wa kilo 4.6 kwa pamoja.
Tukio hilo la ajabu katika Mji wa Musoma na mkoa
kwa jumla, liliwavutia hisia za wananchi hali iliyosababisha msongamano
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa madhumuni ya kutaka kushuhudia.
Akizungumza katika wodi ya wazazi hospitalini
hapo, muuguzi wa zamu, Naabu Geraruma alisema mwanamke huyo alijifungua
juzi saa saba usiku kwa njia ya upasuaji.
Geraruma alisema tukio hilo ni la kwanza katika
hospitali hiyo na hali ya afya ya mzazi huyo na watoto inaendelea vizuri
na muda wowote atahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.
Kwa upande wake, Mganga wa Idara ya Magonjwa ya
Wanawake, Dk Simon Kamuli alisema baada ya jitihada za kuhakikisha
mwanamke huyo anajifungua salama kukamilika, kinachofuatia ni kupelekwa
Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa uangalizi zaidi.
Alisema kuwa hospitali ya mkoa haina uwezo wa
kuwafanya chochote watoto hao, ikiwamo kuwatenganisha na taratibu
zingine kabla ya uchunguzi wa kina.
Post a Comment