Makamanda
shupavu Wanawake wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ ) wakionyesha
umahiri wao katika kulichapa gwaride wakijiandaa na Kilele cha
maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Uwanja wa
Amani Mjini Zanzibar.

Mwenyekiti wa Kamati
ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Balozi Seif akiwa pamoja na
Viongozi wa Kitaifa na Makamanda wa Vikosi vya ulinzi wakiangalia hatua
za matayarisho ya mwisho ya Gwaride litakalopamba kilele cha maadhimisho
ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Uwanja wa Amani Mjini
Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Kaimu Mkuu wa Brigedia Nyuki Zanzibar
Brigedia General Muhaiti na kushoto yake Balozi ni Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d na Katibu
Mkuu Kiongozi Dr. Abdulhamid Yahya Mzee.

Vijana wa Muziki wa
Kikazi Kipya Zanzibar wakiimba wimbo maalum utakaoburudisha kwenye
sherehe za maadhimisho ya Kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar
Januari 12 Uwanja wa Amani. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Matayarisho ya mwisho
kwa ajili ya kilele cha maadhimisho ya kusherehekea kutimia miaka 51 ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yamefikia hatua ya mafanikio
makubwa katika kukamilika kwake.
Maadhimisho hayo
yaliyoanza Tarehe Pili Januari 2015 kwa usafi wa mazingira, uzinduzi
pamoja na uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi mbali mbali ya Taasisi za
Umma na zile binafsi yakiwemo mashindano ya michezo na burdani tofauti
yanafikia kilele chake Januari 12 siku ambayo wakwezi na Wakulima
walijikomboa kutoka katika makucha ya wakoloni.
Vikosi vya ulinzi na usalama vya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na
vile vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vilikamilisha matayarisho ya
mwisho ya Gwaride rasmi hapo Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar
linalotarajiwa kupamba maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na baadhi ya Viongozi wa
Kamati 10 zilizopewa jukumu la kusimamia maandalizi ya sherehe hizo
walishuhudia gwaride la vikosi hivyo vinavyoonekana kuwiva katika
kiwango kilichokusudiwa.
Vikosi vya Jeshi la
Wananchi wa Tanzania { JWTZ }, Polisi, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo {
KMKM }, Mafunzo,Jeshi la Kujenga Uchimi { JKU }, Kikosi cha Zimamoto na
Uokozi na Valantia vilionekana kuupamba uwanja wa amani kwenye
matayarisho hayo vikiwa tayari kwa ajili ya Kilele cha maadhimisho hayo.
Gwaride hilo
lililoongozwa na Luteni Kanali Moh’d Khamis Adam liliambatanisha pia na
matayarisho mengine ya mwisho ya ngoma za utaduni pamoja na muziki wa
Kizazi kipya watakaopata fursa ya kutoa burdani kwenye kilele cha
maadhimisho hayo ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza na
Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa katika Ukumbi wa
Watu mashuhuri { VIP } uliopo Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar mara baada
ya kuangalia matayarisho hayo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Balozi Seif
aliyapongeza majeshi yote kwa hatua yaliyochukuwa ya kushiriki vyema
kwenye maandalizi ya sherehe hizo.
Balozi Seif alisema
juhudi zilizoonyeshwa na wapiganaji hao katika kulichapa gwaride
zimeonyesha wazi umahiri wao katika kutekeleza vyema majukumu
wanayopangia na Taifa.
“ Nimeridhika na
maandlizi yote yaliyochukuliwa na Kamati zote zilizoshiriki
kikamilifu katika matukio mbali mbali tokea sherehe zetu zilipoanza
Mapema mwezi huu. Mambo mazuri sana licha ya kasoro ndogo ndogo
zilizojitokeza ambazo uwezo wa kuzikamilisha upo “. Alisema Balozi Seif.
Mapema Katibu wa
Kamati ya Sherehe na Maadshimisho ya Kitaifa Dr. Khalid Salum Moh’d
alisema Kamati imeandaa utaratibu kwa Wananchi watakaokosa kuingia ndani
ya Uwanja wa Amani kuziona sherehe hizo kupitia TV maalum
zitakazowekwa upande wa jukwa la mashariki { Maarufu jukwaa la Urusi }.
Dr. Khalid alisema TV
hizo zimeandaliwa kwa lengo la kupunguza msongamano mkubwa unaoweza
kutokea endapo wananchi watajitokeza kwa wingi kuhudhuria sherehe hizo
za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 51.
Wageni wa Kimataifa
wapatao 120 miongoni mwao wakiwemo Mabalozi 80 wa Nchi za Nje waliopo
Tanzania wamethibitisha kuhudhuria sherehe hizo, waandishi wa Habari
160 wataripoti matukio ya sherehe hizo wakati vituo vya TV Vinne na
Redio 6 vinatarajiwa kutangaza moja kwa moja sherehe hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Post a Comment