Dk. Kigwangalla akitahadharisha CCM kutokiuka misingi yake

Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Hamis Kigwangalla, ambaye alitangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao, ameitahadharisha CCM kuwa iwapo itakiuka misingi iliyojijenga, nchi itaparaganyika.
Dk. Kigwangalla ambaye pia ni Mbunge wa Nzega (CCM) ametoa tahadhari hiyo jana katika taarifa yake ya salamu za mwaka mpya kwa Watanzania ambayo ameisambaza kwa vyombo vya habari.

“CCM ni lazima tuamke kutoka kwenye raha ya kujiamini ,tusipogutuka sasa tusijeshangaa kuangukia pua bila kutegemea,tuwe na ndoto na matumaini ya Watanzania kwenye moyo na kwenye vichwa vyetu na kuongeza mapinduzi ya kiuchumi na ya kijamii,”alisema na kuongeza kuwa CCM ni chama kinachokubali kuongoza mabadiliko kiuongozi na fikra.

Aliongeza kuwa amani na utulivu vitadumu endapo viongozi wataimarisha utawala bora na kuendelea kuheshimu ubinadamu na utu wa kila mmoja bila kujali hali zao za kiuchumi.

SAKATA LA ESCROW
Dk.Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa alisema sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, imekuwa somo kwa serikali na kwamba inahitaji uzalendo miongoni mwa watumishi wa umma na jinsi wanavyoweza kustawisha misingi ya uwajibikaji na kuweka nidhamu ya kazi.

Dk.Kigwangalla akizungumzia kuhusu katiba inayopendekezwa alisema haina umakini wa kimungu kama ilivyo Qur’an na Biblia kwasababu imeandikwa na wanadamu hivyo inaweza kuwa na makosa na mapungufu  hivyo wanaoilalamikia wasikilizwe kubaini nini cha kufanya.

Alisema siyo sahihi kudai kuwa katiba inayopendekezwa haina mapungufu na pia siyo sahihi kusema  katiba inayopendekezwa ni mbaya kuliko ya mwaka 1977.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Post a Comment

Previous Post Next Post