Escrow yageukia vigogo wengine

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Zoezi la upigwaji kura ya maoni dhidi ya Katiba inayopendekezwa ambalo limepangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu sasa ni dhahiri kwamba liko katika njia panda.
 
Suala hilo lipo njia panda kutokana na maelezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bungeni jana, kwamba zoezi hilo linategemea uwezo wa Tume wa kukamilisha uandikishaji wa wapigakura kwenye daftari la kudumu.
 
Msimamo huo ulitolewa jana na Waziri Mkuu, Pinda wakati akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni, ikiwa ni baada ya kuulizwa swali na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwenye daftari la Kudumu kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) linakamilika kwa kushirikisha wadau wote.
 
Mbowe alisema anazo taarifa kwamba Serikali imekuwa ikikosa fedha za kuandikisha wapigakura kwa mfumo huo na kulazimika kuahirisha zoezi hilo mara kwa mara na mpaka sasa zoezi hilo halijaanza huku ikiwa imesalia miezi mitatu tu kuifikia siku iliyopangwa kwa ajili ya kupiga kura ya maoni.
 
Mbowe alisema kuwa Serikali ilitangaza kwamba zoezi la kuanza kuandikisha wapiga kura kwa utaratibu wa BVR ungeanza Februari, 2014, lakini utaratibu huu haukuanza, ikatangaza tena kuwa itaanza Septemba, 2014, kazi hiyo haikuanza, Kisha tena Serikali ikasema itaanza Desemba, 2014, kazi hiyo haikuanza na  hatimaye ikatangaza kuwa itaanza kazi hiyo Januari 30 yaani leo na kazi hiyo haitaanza.
 
Alisema mara zote hizo Serikali ilikuwa ikiahirisha zoezi la kuanza kuandikisha wapigakura kwa sababu ya ukosefu wa fedha na sasa Tume imesema itaaza kuandikisha wapigakura nchi nzima tarehe 15 Februari mwaka huu, ambapo pia ana shaka kwamba fedha zitakuwapo.
 
Mbowe alisema kuwa wakati taifa likiwa linaahilishwa kila siku kuhusu lini utaratibu huu unaanza, Tume ya Uchaguzi iliomba kuletewa kits  kwa ajili ya uandikishaji 15,000 Serikali ikasema haina uwezo katika hatua hiyo na baadaye ikasema itatoa kits 8000, ambazo  pia hazijafika  nchini.
 
Alisema kuwa kilichojitokeza ni wakati wa majaribio zilitolewa kits 250 ambazo zilifanyiwa majaribio  katika jimbo la Mlele mkoani Katavi, Jimbo la Kilombero, Morogoro na Kawe jijini Dar es Salaam, majaribio ambayo yalionyesha kuwa mitambo hiyo ina matatizo makubwa na kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa wadau kwamba mfumo mzima wa Biometric haujafahamika.
 
“Serikali imetangaza tarehe 30 Aprili kuwa siku ya kura ya maoni, kura ambayo inategemea kutumia daftari hili, ambayo ni miezi mitatu kamili kuanzia sasa hivi, alafu wakati huo huo Uchaguzi Mkuu ni miezi minane kuanzia sasa hivi, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba daftari hili linaandikishwa na wadau wanashirikishwa kikamilifu kwa sababu utaratibu huu ni mpya ili kuliepusha taifa na machafuko ambayo yanaweza kutokana na mizengwe ambayo ilijitokeza wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa?” alihoji Mbowe.
 
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Pinda alianza kwa kukubaliana na Mbowe kwamba mchakato huo umekuwa na matatizo makubwa kifedha ingawa kwa saa Serikali  tayari imepata fedha na iko tayari kutekeleza mpango huo wa kuandikisha wapigakura kwenye daftari la kudumu.
 
Alisema kuwa Serikali imekuwa ikilifanyia kazi suala hilo kwa bidii kubwa ili kuhakikisha kuwa lengo la kuandikisha wapigakura kwenye daftari la kudumu linatimia.
 
“Ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbowe ni kwamba ratiba tuliyopewa na Tume ili kuwezesha mchakato huo kukamilika na zoezi lile kufikia tamati likiwa katika hali nzuri na kuwahakikishia Watanzania kwamba zoezi limefanyika vizuri, ndiyo sasa hivi inayotuongoza, kwa hiyo tunaamini kabisa kwa ratiba hiyo waliyotupa, na sisi tumeshaanza kudepost funds ili kuhakikisha tunakoenda na phase wanayoitaka, kulingana na mpango walivyouweka wao wenyewe, mimi naamini zoezi hili litakamalika kama Tume inavyotaka,” alisema Pinda.
 
Alisema kuwa kinachohitajika hivi sasa ni lazima kuwapo na ushirikishwaji wa wadau wote hasa viongozi wa vyama vya siasa ili kufikia makubaliano ya utekelezaji wa malengo hayo.
 
“Tunachoomba sasa ni Tume kukaa na viongozi wa vyama vya siasa katika kila hatua ili waweze kuakikishiwa kuwa  ni namna gani mchakato unavyokwenda, tukifanya hili nadhani linaweza likatupa comfort kubwa,” alisema Pinda.
 
Aidha Pinda alisema kuwa vifaa vya BVR 250 vilivyoletwa nchini vilikuwa ni kwajili ya kupima uwezo wake ili kuwa na uhakika kwamba havitaleta mgogoro wakati wa utendaji.
 
Alisema kuwa baada ya vifaa hivyo kuwasili, Serikali iliwataka watengenezaji wa vifaa hivyo waje nchini na walikuja kwa ajili ya kushiriki majaribio ya vifaa hivyo.
 
Pinda alikiri kuwa ni kweli  kulibainika matatizo ya hapa na pale ya kitaalam ambayo waliwataka wayarekebishe ili vifaa hivyo viweze kufanya kazi kwa ufanisi.
 
“Lakini kwa sehemu kubwa vifaa vile vilionekana uwezo wake na capacity yake, yaani uwezo wake wa kuandikisha Watanzania kwa siku ni mara mbili ya kile tulichokuwa tumefikiria hapo awali, kwa maelezo haya ni imani yangu kwamba zoezi litakwenda vizuri kwa muda unaotakiwa na tulitumia daftari hilo katika kura ya maoni na baadaye kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Pinda.
 
Katika swali lake la nyongeza, Mbowe alisema kuwa kuanzia sasa zimebaki siku 90 kuelekea kwenye kura ya maoni na kwamba wanasiasa siyo wataalam wa masuala ya IT, na walitegemea kuwa wadau wangeshirikishwa kuanzia namna ambavyo mfumo huo unavyofanya kazi, lakini inavyoonyesha ni kwamba Serikali inajua na kama Serikali inajua maana yake ni kwamba Chama Cha Mapinduzi kinajua hali ambayo inaonyesha kuwa wapinzani hawatashirikishwa vya kutosha.
 
Aidha, Mbowe alisema kuwa katika majaribio imeonyesha kuwa vifaa hivyo vinao uwezo wa kuandikisha watu 22 kwa siku na kwamba kutokana na idadi kubwa ya Watanzania wenye sifa ya kuandikishwa muda hautatosha.
 
Mbowe alimtaka Waziri Mkuu kuutangazia umma wa Watanzania kwamba Tume itatoa muda wa kutosha wa kujiandikisha badala ya kutumia utaratibu wa haraka haraka aliouita ‘Vodafasta’ ili wananchi wapate haki yao ya msingi ya kupiga kura.
 
Mbowe alisema hata watu wanaotarajiwa kutumika kuandikisha wapigakura, baadhi yao ni watumishi wa Serikali ambao wengi wao hawana uelewa wa IT, hivyo akapendekeza zoezi la kura ya maoni liahirishwe.
 
Akijibu swali hilo, Pinda alisema kuwa anaheshimu mawazo ya Mbowe na asingependa kubishana naye huku akisema kuwa anachosema kinatokana na maelezo aliyopewa na Tume, lakini akasema kuwa ikiwa itabainika kwamba suala hilo haliwezekani atarejea tena bungeni na kueleza. 
 
Hivi karibuni, baadhi ya wanasiasa, wananzuoni, viongozi wa dini na wadau mbalimbali wamekuwa wakiishauri Serikali kuahirisha zoezi la kupiga kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa madai kuwa hakuna maandalizi ya kutosha.
 
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema kuwa suala la kupiga kura ya maoni Aprili 30, mwaka huu ni ndoto kutokana na kusuasua kwa maandalizi ya suala hilo, huku kukiwa hakuna mikakati yoyote iliyofanyika ya kuwapatia wananchi elimu.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post