Moshi. Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta jana alipanda
kizimbani kutoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Hai tukio
lililovuta hisia za wananchi wengi kwani ni la kwanza na la aina yake
kwa kiongozi wa juu wa mhimili huo wa dola.
Jaji Samatta aliingia eneo la Mahakama saa 2.40
asubuhi akifuatana na Profesa Abdallah Safari na baadaye kwenda moja kwa
moja chumba cha mapumziko kabla ya kuingia mahakamani.
Baada ya kula kiapo kutoka kwa karani wa Mahakama
hiyo, Baltazar Buretta, Jaji Samatta alianza kutoa ushahidi katika kesi
inayomkabili Adam Abeid (25) ya kujifanya jaji huyo na kutaka kuwatapeli
viongozi wa Chadema, akisema alishtuka alipoelezwa na Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa kuwa kuna mtu ambaye amempigia simu
akijitambusha kuwa ni Jaji Samatta.
Abeid pia anakabiliwa na shtaka kutaka kumtapeli Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa ilisikilizwa chemba huku Jaji Samatta
akiongozwa kutoa ushahidi wake na Mwanasheria wa Takukuru, Susan Kimario
anayesaidiana na Furahini Kibanga akikana kumfahamu wala kuwa na
uhusiano na mshtakiwa huyo.
Jaji Samatta ambaye sasa ni Mkuu wa Chuo Kikuu
Mzumbe na mjumbe wa Bodi ya Kuchuja Mahakimu na Majaji Kenya, alisema
kati ya Aprili na Mei 2012, Dk Slaa alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi
(sms) akiambatanisha na ujumbe unaodaiwa kutumwa na mshtakiwa, akimtaka
athibitishe kama ndiye aliyeutuma kwake.
Ujumbe huo ulisomeka: “Hali yako Dk Slaa, kesho
nataka nikamuone Jaji Mkuu Chande, naomba nichangie nauli (ili)
nikashughulikie yale masuala yetu.”
Jaji Samatta alisema alishtuka na kuamua kumpigia
simu Dk Slaa na kumweleza kuwa ujumbe huo haukuwa umetoka kwake na
kumtaka alifikishe suala hilo kwenye vyombo vya dola.
“Nilimpigia pia Wakili Profesa Safari (Abdallah)
nikamuomba ahakikishe suala hilo haliishi kisiasa, bali upelelezi
ufanyike kwa sababu hadhi yangu na heshima yangu ilikuwa at stake
(shakani),” alisema.
Maswali kati ya mshtakiwa na Jaji Samatta yalikuwa kama ifuatavyo;
Mshtakiwa: Je, katika zile meseji alizokutumia Dk Slaa unazo kwenye simu yako?
Jaji Samatta: Zile meseji ziko katika simu yangu ya zamani ambayo niliacha kuitumia baada ya kuzeeka.
- Mwananchi
- Mwananchi

Post a Comment