Jinsi bendi ya walemavu inayokubalika nchini

Nimekutana na watu wengi wakidai kuwa wana tatizo fulani linalowafanya washindwe kuonyesha uwezo wao kwenye kazi fulani, wengine wakikimbia kuomba, kuwa tegemezi kwa madai kuwa ni walemavu.
Ulemavu siyo kikwazo cha kushindwa kutekeleza majukumu ya msingi ya kila binadamu ingawa wakati mwingine ni changamoto.
Changamoto hiyo na nyingine nyingi wanakutana nazo watu wenye walemavu zimefanyiwa kazi na wanamuziki wa Bendi ya Tunaweza ambao kwa ujumla wao ni walemavu wa viungo, lakini kila mmoja anaonyesha kipaji chake kadri awezavyo.
Wanamuziki wa bendi hii walikutana mwaka 2008, wakikusanywa na Masudi Wanani na kuanzisha bendi hiyo iliyokuwa na wanamuziki 10 na walikuwa wanafanyia mazoezi eneo la Mkwizu kwa mafundi magari, Magomeni jijini Dar es Salaam.
Mtayarishaji wa muziki wa bendi hiyo, Kudra Mazongela anawataja wanamuziki waanzilishi wa bendi hii, kiongozi wao Idd Tembo, Salehe Abdallah akiwa ndiye dansa, Mwakatobe Peter analikung’uta gitaa la solo na Emannuel Mpesa anapiga kinanda.
Mazongela anasema kuwa yeye mwenyewe pamoja na kuimba pia ni mpiga gitaa la bezi, wanamuziki wengine walioanzisha bendi hiyo ni Irene Malekela na Latifa Abdallah ambao ni waimbaji.
Anasema waliendelea kujifunza kwa kuhama hama kutokana na kukosa eneo maalumu la kufanyia mazoezi hadi walipofanikiwa kurekodi albamu yao ya kwanza yenye jina la ‘Raha Duniani’.
Anazitaja nyimbo zilizokuwamo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Raha Duniani’, ‘Tutenge’, ‘Mbilimbi’, ‘Kokolido’, ‘Walemavu Tuungane’ na ’Tunamshukuru Mungu’.
Mazongela anafafanua kuwa nyimbo zote za albamu hiyo zinawagusa watu wenye matatizo ambao wanahitaji kupewa moyo au kujitambua na kukataa kubweteka kwa kujichanganya kutafuta maisha.
Anatolea mfano wimbo wa ‘Walemavu Tuungane’ lengo lake ni kuwakumbusha kwamba wanatakiwa kuwa kitu kimoja ili iwe rahisi kuwezeshwa kwani kwa umoja wao wanaweza kufanya vitu vya ajabu kuliko wakigawanyika.
Mazongela anafafanua kuwa wimbo wa ‘Tunamshukuru Mungu’, lengo lake ni kuwakumbusha waja wote kuwa wanatakiwa kushukuru kwa hali yoyote waliyokuwa nayo cha msingi bado roho inadunda.
“Tumeungana na hadi sasa tupo pamoja, tukiwezeshwa tunaweza kwa sababu kila mmoja anakubali hali aliyokuwa nayo, kumshukuru Mungu katika hili ni lazima kwani ukiwa unalia huna miguu kuna mwingine hana hata mdomo wa kuonyesha kuwa analia hivyo hata akilia hakuna anayejua,” anasema Mazongela

Post a Comment

Previous Post Next Post